Habari Mseto

Aua mkewe kwa kukataa kumpikia ugali

February 19th, 2019 1 min read

Na BENSON AMADALA

MWANAUME aliyemuua mkewe kwa kukataa kumpikia ugali, amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi cha Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kakamega baada ya kunywa sumu.

Mauaji hayo yalitokea kijijini Emukaba, Butsotso, Kaunti ya Kakamega na majirani walida yalitokana na mzozo ulioibuka baada ya mwendazake kukataa kumpikia ugali mshukiwa.

Mshukiwa mwenye umri wa miaka 45, anadaiwa kukasirishwa na hatua hiyo ya mwendazake hivyo akamshambulia kwa kisu na kumdunga mara kadhaa.

Baada ya kumuua, mshukiwa anadaiwa kufunika maiti kwa blanketi ili kuficha ushahidi. Baadaye alienda kutazama mashindano ya kupigana kwa fahali kijijini hapo.

Aliporejea nyumbani muda mfupi baadaye, majirani kwake walipata mwili wa mwendazake umefichwa ndani ya blanketi na mshukiwa amezimia baada ya kumeza sumu.

Majirani baadaye waliwaita polisi ambao tayari wameanzisha uchunguzi kuhusiana na kisa hicho.

“Mshukiwa alijaribu kujiua kwa kunywa sumu na alikimbizwa hospitalini kwa ajili ya matibabu,” akasema Afisa Mkuu wa Polisi (OCPD) wa Kakamega Joseph Chebii.

Be Chebii alisema mshukiwa atafikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka ya mauaji atakapopata nafuu.

Mshauri wa Masuala ya Kijinsia na Mipango Maalumu wa Kaunti ya Kakamega, Peninah Mukabane alielezea masikitiko yake kuhusiana na ongezeko la mizozo ya kinyumbani katika eneo hilo.

“Kumekuwa na ongezeko la mizozo ya kinyumbani kutokana na matumizi ya dawa za kulevya,” akasema Bi Mukabane.

Alisema kuwa idara yake imeanzisha mikakati ya kushughulikia mizozo ya kinyumbani miongoni mwa wakazi wa kaunti hiyo.

Katika eneo la Shiyunzu, mwanaume mwingine wa umri wa miaka 30 aliaga dunia alipokunywa sumu mara baada ya kutembelea wakwe zake kutatua mzozo baina yake na mkewe.

Bw Chebii alisema mwanaume huyo alizimia na kufariki papo hapo. Maiti yake imehifadhiwa katika mochari ya hospitali ya Kaunti ya Kakamega na polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusiana na kisa hicho.