Habari Mseto

Aua mkewe kwa kupokea simu ya dume lingine

June 26th, 2018 1 min read

Na BENSON AMADALA

MWANAMUME alimshambulia mke wake kwa panga katika kijiji cha Shivakala, Kaunti ya Kakamega, na kumuua kwa kupigiwa simu na mwanamume mwingine usiku wa kuamkia Jumatatu.

Mwanamke huyo aliyetambuliwa kama Doreen Masinde, alikimbizwa hadi katika Hospitali ya Rufaa ya Kakamega baada ya kukatwa mkono wa kushoto na mume wake, lakini akafariki kwa kuvuja damu nyingi.

Mkuu wa polisi wa eneo hilo, Bw Bernstein Shari, alisema mwanamume huyo alikamatwa na atashtakiwa.

Ilisemekana alimshambulia mke wake mwenye umri wa miaka 21 baada ya kupokea simu kutoka kwa mwanamume mwingine usiku.

“Mwanamume huyo alishuku kuwa mkewe alikuwa na mpenzi wa kando ndipo akamshambulia na kumkata mkono”, akasema Bw Shari.

Polisi walimkamata mshukiwa na wakapata upanga uliotumiwa katika mauaji hayo.

“Mshukiwa atafikishwa mahakamani wakati uchunguzi utakapokamilika”, akasema mkuu huyo wa polisi.

Kwingineko katika kijiji jirani cha Shikwato, lokesheni ndogo ya Malinya, mhudumu wa bodaboda alikamatwa kwa kushukiwa kumnajisi mtoto wa miezi 17.

Mamake mtoto huyo alikuwa amemwachia wifi yake mtoto huyo alipoenda kuhudhuria mkutano wa kikundi cha wanawake kijijini.

Aliporejea mwendo wa saa kumi na mbili jioni Jumapili, alimwona mshukiwa akitorokea shamba la mahindi lililo karibu.

Mwanamke huyo alipiga kemina wanakijiji wakafanikiwa kumkamata mshukiwa aliyekuwa akijaribu kutoroka.

Walipoingia ndani ya nyumba walimpata mtoto amepoteza fahamu kitandani huku kukiwa na madoa ya damu kwenye shuka zilizokuwa zimetumiwa kumfunika.

Bw Shari alisema wametuma maombi ili waruhusiwe kukusanya chembechembe za mwili wa mshukiwa kuwawezesha kukamilisha uchunguzi.

‘Hiki ni kisa cha kusikitisha sana ambacho hakiwezi kunyamaziwa. Mshukiwa huenda alitumia nafasi ya kuona hapakuwa na watu nyumbani kuingia na kumnajisi mtoto,” akasema.