Habari Mseto

Auawa kwa kulewa divai na kuiba sadaka kanisani

August 21st, 2018 1 min read

Na Steve Njuguna

MSHUKIWA wa wizi Jumamosi aliuawa na wananchi katika eneo la Ndaragwa, Kaunti ya Nyandarua baada ya kudaiwa alivunja lango la kanisa na kuiba sadaka.

Kulingana na wanakijiji, mwanaume huyo kwa ujasiri mkubwa alivunja lango la kanisa hilo saa sita usiku, akaingia ndani na kuiba sadaka kisha akazima kiu chake kwa kunywa divai iliyohifadhiwa hadi akalewa chopi.

“Tunashuku kwamba mshukiwa alikunywa divai hadi akalewa chakari kabla ya kupatwa na usingizi mzito na akalala kanisani bila ufahamu wake,” akasema mwanakijiji, Joseph Muriuki. Kulingana na Bw Muriuki Ilipofika asubuhi, majirani waliosikia kishindo kanisani walipiga kamsa iliyowavutia watu wengine.

“Wanakijiji walioitikia kamsa hizo walipata mshukiwa akijaribu kutoroka. Hapo ndipo walimpa kipigo kikali hadi akafa,” akasema mwanakijiji mwengine Hanna Wamuyu.

Afisa wa polisi aliyefika katika eneo la tukio kumwokoa marehemu alipata tayari ashakata roho.