Michezo

Auba akiyoyomea Real, nitaenda Atletico – Lacazette

June 4th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

ALEXANDRE Lacazette wa Arsenal amekataa ombi la kusajiliwa na Inter Milan ya kocha Antonio Conte mwishoni mwa msimu huu.

Inter ambao hushiriki Ligi Kuu ya Italia (Serie A), wanatafuta kizibo cha fowadi Lautaro Martinez ambaye kwa sasa yuko pua na mdomo kutua Barcelona, Uhispania.

Lacazette ambaye mkataba wake na Arsenal unatamatika rasmi mwishoni mwa msimu wa 2021-22, hajakuwa na uhakika wa kupangwa katika kikosi cha kwanza cha Arsenal chini ya mkufunzi mpya Mikel Arteta.

Yalikuwa matarajio ya Inter kwamba nyota huyo mzawa wa Ufaransa angalikuwa mwepesi wa kujiunga nao kwa sababu hiyo ya kutowajibishwa vilivyo na Arteta.

Barcelona wako radhi kuweka mezani kima cha Sh14 bilioni kwa minajili ya Martinez anayetazamiwa kuchukua nafasi ya kigogo Luis Suarez uwanjani Nou Camp.

Kwa mujibu wa gazeti la ‘Equipe nchini Ufaransa, Inter walinuia kutumia Sh9 bilioni kumshawishi Lacazatte kubanduka Emirates na kutua ugani San Siro.

Hadi kufikia sasa, Lacazette anajivunia kufunga mabao tisa na kuchangia matatu kutokana na mechi 26 zilizopita za Arsenal. Mfumaji huyo wa zamani wa Olympique Lyon, anahusishwa na uwezekano wa kuyoyomea Atletico Madrid kujaza nafasi ya Thomas Partey anayewindwa na Arsenal usiku na mchana.

Ingawa hivyo, Arteta ameshikilia kwamba matamanio yake ni kuendelea kujivunia huduma za Lacazette na kumtumia kama mvamizi mkuu baada ya nahodha Pierre-Emerick Aubameyang kufichua azma ya kutua Real Madrid, Uhispania.

Lacazette alijiunga na Arsenal mnamo 2017 baada ya kuagana na Lyon ya Ufaransa kwa kima cha Sh6.5 bilioni.

Mpango huo ulifichuka saa chache baada ya Arsenal kufuta kazi maskauti 10 waliotambua vipaji vya chipukizi Bukayo Saka, Ainsley Maitland-Niles na Reiss Nelson na hatimaye kushawishi usimamizi wa kikosi hicho cha EPL kuwasajili.

Wahudumu wengine ambao Arsenal imelazimika kuwatema baada ya hazina yao ya fedha kutikiswa na janga la corona ni vibarua ambao mikataba yao ilikuwa itamatike rasmi mwishoni mwa Juni 2020.

Licha ya maamuzi hayo, Arsenal wamesisitiza kwamba wataridhia kuwaajiri upya wafanyakazi wao wote walioagana nao kutokana na corona baadaye mwaka huu au pindi janga hilo litakapodhibitiwa vilivyo.

Makinda wengine waliotambuliwa na maskauti hao chini ya Steve Morrow aliyekuwa kinara wa usajili wa chipukizi, ni Joe Willock na Eddie Nketiah.

Msimu jana, Arsenal walitia kapuni zaidi ya Sh7 bilioni kutokana na mauzo ya Alex Iwobi na Krystian Bielik waliowahi kuwa makinda wao wa akademia. Waliyoyomea Everton na Derby County mtawalia.