Michezo

Aubameyang ampongeza Cech kwa kuwaokoa dhidi ya Everton

September 24th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

FOWADI wa Arsenal Pierre-Emerick Aubameyang amemsifu kipa veterani Petr Cech kwa kuokoa mipira mingi ya hatari langoni wakati wa mechi yao ya Ligi kuu ya Uingereza (EPL) dhidi ya Everton ugani Emirates Jumapili Septemba 23, mechi waliyoishinda mabao 2-0.

“Nafikiri kwa zaidi ya mara 20, mnyakaji wetu  Petr Cech alituweka mchezoni. Tunaendelea kuimarika kila kukicha na tunahisi vizuri tunapootwaa ushindi haswa dhidi ya timu zinazotoa upinzani mkali kama Everton. Mambo ni nywee kwa vile tunafurahia mazoezini chini ya kocha mpya,” akasema Aubameyang.

Kufuatia ushindi huo ‘The Gunners’ wanazidi kuimarika ingawa walianza msimu vibaya kwa kujikwaa dhidi ya majabali Manchester city na Chelsea kisha wakajisuka na kurejea kwa matao ya juu, ushindi wa Jumapili ukiwa wa tano baada ya kujibwaga uwanjani mara saba.

Ingawa mashabiki wa Arsenal wamekuwa wakimtaka kocha Unai Emery kumwanzisha nyani  mpya Bernardo Leno, straika huyo alisema kiwango cha uchezaji wa Cech ni dhihirisho tosha kwa uaminifu alionao kocha kwake mchumani.

Vile vile straika huyo raia wa Gabon alisifu ushirikiano mpya wa kuhusudiwa kati yake na  mshambulizi raia wa Ufaransa Alexandre Lacazatte aliyefungia Arsenali bao la kwanza katika mechi dhidi ya Everton.

“Nimekuwa na uhusiano wa kupigiwa mfano na Lacazette tangu nilipotua kambini mwa Arsenal. Tunafurahikia ushiriikiano wetu na kila moja wetu anajua wakati wa kukimbia ili kumegewa pasi,” akafafanua  Aaubameyang.