Michezo

Aubameyang ataka Sh35 milioni kwa wiki ndipo arefushe mkataba

July 4th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

MSHAMBULIAJI na nahodha Pierre-Emerick Aubameyang, 31, amewapa waajiri wake Arsenal masharti mapya ya kutimiza kabla ya kutia saini kandarasi mpya uwanjani Emirates.

Fowadi huyo mzawa wa Gabon anataka kupokezwa mkataba mpya wa angalau miaka mitatu utakaomshuhudia akilipwa mshahara wa hadi Sh35 milioni kwa wiki badala ya ule wa sasa wa Sh28 milioni mwishoni mwa kila juma.

Kiungo Mesut Ozil ambaye anadumishwa na Arsenal kwa mshahara mkubwa zaidi uwanjani Emirates, anapokezwa mshahara wa Sh49 milioni kwa wiki.

Aubameyang ambaye anapigiwa upatu wa kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa msimu wa pili mfululizo, yuko katika mwaka wa mwisho wa mkataba wake na Arsenal.

Kwa mujibu wa kocha Mikel Arteta, Arsenal wanasubiri kujua iwapo watafuzu kwa soka ya bara Ulaya (Europa League) muhula ujao kabla ya kutathmini uwezekano wa kutimiza baadhi ya masharti ya Aubameyang ambaye pia anawaniwa na Barcelona, Inter Milan, Juventus, Chelsea na Real Madrid.

Hadi atakapowangoza Arsenal kupepetana leo Jumamosi na Wolves uwanjani Molineux, Aubameyang tayari amepachika wavuni mabao 19 kutokana na mechi 32 za EPL msimu huu.

Mabao mawili aliyofunga dhidi ya Norwich City mnamo Julai 1, 2020, yalimweka Aubameyang katika rekodi ya kuwa mwanasoka wa kwanza kupachika wavuni mabao 50 ya EPL haraka zaidi.

Kuondoka kwake huenda kukamchochea pia mfumaji Alexandre Lacazette kuyoyomea Atletico Madrid ya Uhispania na nafasi yake kutwaliwa na mwanasoka Thomas Partey wa Atletico. Lacazette alisajiliwa na Arsenal mnamo Julai 2017 kutoka Olympique Lyon ya Ufaransa.