Aubameyang kutua Real Madrid kutimiza ahadi aliyompa marehemu babu yake

Aubameyang kutua Real Madrid kutimiza ahadi aliyompa marehemu babu yake

Na CHRIS ADUNGO

MSHAMBULIAJI Pierre-Emerick Aubameyang amewapa mashabiki wa Arsenal kidokezi tosha kwamba muda wake wa kuhudumu uwanjani Emirates kimekaribia kutamatika.

Katika mahojiano yake na gazeti la The Sun mnamo Mei 10, 2020, nyota huyo mzawa wa Gabon alisema kwamba anatawaliwa na kiu ya kutimiza ahadi ya kuchezea Real Madrid kwa kuwa ndiyo maneno ya mwisho aliyomwambia babu yake kabla yake kuaga dunia.

Akihojiwa na gazeti la Mirror Sport mnamo 2016 – akichezea Borussia Dortmund wakati huo – Aubameyang aliungama kuwa aliwahi kumtolea ahadi babu yake kwamba atachezea Real siku moja kabla ya kustaafu kwenye ulingo wa soka.

Aidha, alifichua kwamba mtindo wake wa kusherehekea mabao kwa kupiga kichwangomba (somersaults) ni katika juhudi za kuiga aliyekuwa nguli wa soka uwanjani Santiago Bernabeu, Hugo Sanchez.

“Kabla ya kuaga dunia miaka miwili iliyopita, niliahidi babu yangu kwamba nitakuja kuwachezea Real siku moja. Yeye alikuwa mzawa wa Avila, mji mdogo uliopo karibu na Madrid, Uhispania,” Aubameyang akatanguliza.

“Najua hayatakuwa maamuzi rahisi ila nahisi kwamba sitapata kabisa utulivu iwapo nitakataa kutimiza ahadi hiyo niliyotoa. Itakuwa vibaya nikisalia kudaiwa na nafsi yangu siku zote za maisha haya,” akaongeza.

“Nasherehekea mabao yangu kwa kuiga Hugo ambaye nilianza kumfuatilia tangu utotoni na kuzitazama video zake mtandaoni,” akasema.

Sanchez ambaye ni mzawa wa Mexico, aliwahi kufungia Real jumla ya mabao 208 kutokana na mechi 283 na kusaidia kikosi hicho kutwaa mataji matano ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kati ya 1985 na 1992.

Kwa upande wake, Aubameyang alijiunga na Arsenal mnamo Januari 2018 na anajivunia kupachika wavuni jumla ya mabao 49 kutokana na mechi 75 zilizopita. Hadi kufikia sasa msimu huu, ametikisa nyavu za wapinzani mara 17 na ni miongoni mwa wafumaji wanaopigiwa tena upatu wa kutwaa taji la mfungaji bora wa EPL.

Mkataba wake ugani Emirates unatamatika rasmi mwishoni mwa msimu wa 2020-21 na Arsenal hawapo tayari kumpoteza tena mchezaji mwingine bure bilashi tangu Aaron Ramsey ajiunge na Juventus ya Italia bila ada.

Japo kocha Mikel Arteta ameapa kumsadikisha Aubameyang kusalia Arsenal, huenda kikosi hicho kikashawishika kumuuza kwa Sh4 bilioni badala ya kumkwamilia na asiwaletee lolote la kujivunia.

Mbali na Real, vikosi vingine vinavyomezea mate maarifa ya Aubameyang ni Chelsea, Manchester United, Inter Milan, Atletico Madrid na Barcelona waliojaribu kusajili mwanzoni mwa mwaka huu wa 2020.

“Kuchezea Real au kikosi chochote kingine cha haiba kubwa nchini Uhispania ni kati ya matamanio yangu makubwa. Hiyo itakuwa zawadi kubwa kwa mamangu Margarita Crespo ambaye ni mzawa wa Uhispania,” akasema Aubameyang.

“Aubameyang aliwahi kutoa ahadi kubwa kwa marehemu babu yake. Itakuwa vyema aitimize. Pili, alikuwa shabiki sugu wa Real hata akiwa mtoto mdogo. Alikuwa akifahamu majina ya wachezaji wengi wa Real, si ya Barcelona. Isitoshe, familia yangu nzima ni mashabiki wa Real. Hivyo, itakuwa fahari na tija tele kuona Aubameyang akiwa ndani ya jezi nyeupe za Real,” akasema Margarita.

You can share this post!

Wenger amtunuka sifa chipukizi Kylian Mbappe

Mwatate United FC yafurahia udhamini kutoka kwa Teita...

adminleo