Michezo

Augsburg waduwaza Borussia Dortmund ligini

September 26th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

BORUSSIA Dortmund waliduwazwa na FC Augsburg kwa kichapo cha 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) iliyohudhuriwa na takriban mashabiki 6,000 uwanjani WWK Arena mnamo Septemba 26, 2020.

Felix Uduokhai aliwaweka wenyeji Augsburg kifua mbele kunako dakika ya 40 baada ya kushirikiana vilivyo na Daniel Caligiuri. Bao hilo lilikuwa la kwanza kwa Uduokhai kufunga tangu 2017.

Caligiuri alifungia Augsburg bao la pili katika dakika ya 54 alipokamilisha krosi ya Florian Niederlechner aliyemwacha hoi beki Thomas Meunier wa Dortmund.

Ingawa chipukizi Erling Braut Haaland alijitahidi sana kuwarejesha waajiri wake Dortmund mchezoni, ushirikiano wake na Jadon Sancho anayewaniwa na Manchester United haukuzalisha matunda yoyote na makombora yake mawili yalipanguliwa kirahisi na kipa Rafal Gikiewicz.

Augsburg, ambao sasa wamesajili ushindi katika michuano miwili ya ufunguzi wa msimu huu, walimiliki asilimia 20 pekee ya mpira na mabao mawili waliyoyapata yalitokana na fursa mbili za pekee ambazo walipata langoni pa Dortmund katika dakika 90 za kwanza.

Alfred Finnbogason nusura awafungie Augsburg mabao mawili ya ziada mwishoni mwa muda wa majeruhi ila akanyimwa fursa na kipa Roman Burki.

Mechi hiyo ilikuwa ya tatu kwa chipukizi raia wa Uingereza, Jude Bellingham, 17, kuchezea Dortmund tangu ajiunge nao kutoka Birmingham City. Fowadi huyo aliondolewa ugani katika dakika ya 60.

Kwingineko, Bayer Leverkusen na RB Leipzig waliambulia sare ya 1-1.