Aunda programu inayotoa huduma za mifugo Afrika Mashariki

Aunda programu inayotoa huduma za mifugo Afrika Mashariki

Na SAMMY WAWERU

Mwaka wa 2019 Oscar Ngime ambaye ni mfugaji hodari wa mbwa alipoteza vilebu wanane aina ya German shepherd baada ya kuambukizwa maradhi ya Parvovirus.

Anahoji endapo wangefanikiwa kuwa hai, wana hao wa mbwa wangemuingizia kima kisichopungua Sh250, 000.

Oscar pia hufuga na kujamiisha mbwa aina ya Havanese na Japanese Spitz eneo la Lower Kabete, Kaunti ya Kiambu.

Mfugaji huyu vilevile anakumbuka kisa kingine, ambapo nusra apoteze kasuku wake aliyeuguza majeraha mabaya.

Anasema kupata vetinari ilikuwa kibarua, hasa kufuatia sekta ya mifugo na ufugaji nchini kukumbwa na kero ya ‘maafisa’ na ‘madaktari’ bandia.

“Wana wa mbwa, nilisafiri kilomita 20 ila sikupata daktari. Hatimaye walifariki kutokana na virusi vya Parvo,” Oscar anakadiria hasara.

Kasuku, nyuni mchangamfu na msema mengi, alipata daktari ingawa anasema haikuwa rahisi.

Ni matukio yaliyomfumbua macho ili kuepuka mkumbo sawa na huo siku za usoni, ikizingatiwa kuwa yeye ni kipenzi cha wanyama.

“Baada ya kufanya utafiti niligundua mahangaiko hayo yanafika wakulima na wafugaji wengi,” aelezea.

Kuzindua apu ya Bobbi

Oscar alijituma kutafuta suluhu, kilele kikiwa kukumbatia mfumo wa teknolojia ya kisasa.

Akiutaja kuwa wa kipekee katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla, kupitia usaidizi wa mtaalamu wa masuala ya Habari na Teknolojia alizindua apu, maarufu kama Bobbi.

Aidha, Bobbi ni jina la lakabu linalotokana na Kasuku wake mwenye umri wa miaka saba sasa.

Apu hiyo ni jukwaa la wafugaji kufikia mavetinari na madaktari wa mifugo, na pia kupata soko la bidhaa za ufugaji.

“Ni duka – safu ya pamoja wafugaji kufikia mavetinari na wauzaji wa bidhaa za mifugo, na kusaka soko,” Oscar afafanua.

Apu hiyo inayotumika kupitia simu za kisasa aina ya Android na tovuti, ilimgharimu Sh350, 000 kuizindua.

Kando na huduma hizo, inatoa maelezo ya aliko mkulima – mfugaji, vetinari na wanaouza bidhaa za mifugo, kupitia mapu ya Google.

Isitoshe, Bobbi ina jukwaa la jumbe, yaani mfugaji anapata fursa ya kuwasiliana na vetinari au muuzaji wa bidhaa kwa njia ya maandishi.

Kufungua akaunti na jukwaa la soko

Huduma zingine zinatolewa na apu hiyo ni uuzaji na ununuzi wa ng’ombe, kuku, kondoo, mayai, mbuzi, samaki na wanyama vipenzi wa nyumbani kama vile nyuni.

Kuwa mshirika au memba, unahitaji kujisajili ili kufikia muuzaji au mnunuzi.

“Kimsingi, ni muhimu mfugaji au mkulima apate soko la mazao na bidhaa zake bila hujuma za mabroka,” asisitiza, akisifia utendakazi wa Bobbi.

Ukiwa na simu ya tachi, unajisajili baada ya kupekua mtandao huo kupitia Google Play store.

Bobbi imeunganishwa na tovuti, ambapo unaweza kujisajili, Oscar akidokeza anapanga kushirikiana na Facebook hivi karibuni.

Kufungua akaunti, unapaswa kujaza maelezo binafsi yanayojumuisha; majina, barua pepe (e-mail address), nambari za simu, kisha nambari za siri kuingia mtandaoni.

“Baada ya kuitikia sheria na kanuni zetu, unapata arafa (ujumbe) kutoka kwa bobbi umefanikiwa kujisajili,” mwasisi huyo aelezea, akisema hatua hizo ni za moja kwa moja.

Akihakikishia waliojiunga usalama wa data na maelezo yao, anasema apu hiyo haitozi malipo.

“Hatujaingia ulingo wa biashara,” asema mwanateknolojia huyu mwenye Stashahada Masuala ya Usimamizi wa Biashara.

Usalama wa data

Huku visa vya uchakachuaji na uhalifu mitandaoni vikiendelea kushuhudiwa na kuripotiwa nchini, Oscar anasema Bobbi inatii sheria za Google ili kudumisha usalama wa washirika.

Kufikia sasa, apu hiyo ina zaidi ya wanachama 1, 000 akisema ikikumbatiwa na wafugaji na wakulima italeta afueni, kuimarisha soko na kusaidia kuondoa kero ya mawakala – mabroka.

Ili tangazo au matangazo yaidhinishwe, kupakiwa na kuchapishwa, Oscar ambaye ni adimini hukagua na kuthibitisha kwa kina uhalisia wake.

“Tunahimiza wauzaji, kuambatanisha maombi ya machapisho na picha, bei ya bidhaa, pini – mahali walipo na kuweka wazi ikiwa kuna nafasi ya majadiliano bei kupunguzwa,” afafanua.

Kauli za wataalamu

Memba wengi wanatoka Kenya na Uganda, na kadha Tanzania.

Akisifia ubunifu huo, Samson Ogola, mwanzilishi na mmiliki wa Karabach Media, kampuni inayotoa huduma za mauzo kwa njia ya kidijitali, anahimiza haja ya Bobbi kushirikisha bidhaa zingine za kilimo, kando na huduma za ufugaji pekee.

“Kuna apu nyingi za mauzo, na kuwa na inayolenga wanyama pekee ni wazo la busara. Hata hivyo, ni muhimu mtandao wa aina hiyo uwe pana na kuhusisha bidhaa na mazao ya kilimo.

“Mitandao kama hiyo inaanzishwa ili kutatua changamoto zinazozingira sekta ya kilimo, ufugaji na biashara kwa jumla,” Ogola ashauri, akiongeza kusema, hatua hiyo itafanya Bobbi kuwa na manufaa zaidi.

Naye Dkt Jemimah Njuki, Mkurugenzi Mkuu Africa International Food Policy Research (IFPRI), anahimiza haja ya apu za kusaka soko la bidhaa za ufugaji na mazao ya kilimo kuunganishwa, pamoja na kuzinduliwa zikiwa na uwezo kusitiriwa na/kwenye simu za bei nafuu ili kufikia wakulima wa mapato ya chini na ya kadri.

“Wanazaraa wengi wanaendeleza kilimo-mseto kinachojumuisha ufugaji. Kwa kuunganisha apu zote na kuzifanya kupatikana kwenye simu za bei nafuu, mbali na za Android na Apple, kutawasaidia kuangazia kero ya soko,” asema Dkt Jemimahi, akitaja mianya bora inayotokana na apu hizo.

Changamoto kuboresha bobbi

Safari ya kuboresha bobbi hata hivyo haijakuwa rahisi.

Oscar, 40, anaiambia Taifa Leo Dijitali kwamba kila mwaka hulipa ada ya Sh15, 000 kwa kampuni inayomsaidia kutoa huduma na kiwango sawa na hicho kwa fundi, ikikumbukwa kuwa apu hiyo haijaanza kumuingizia mapato.

“Mwaka uliopita, Google App Store ilikuwa imesimamisha na kuondoa bobbi kwenye intaneti kwa madai tulikiuka sheria. Hata hivyo, tulisuluhisha na sasa tuko ngangari kuendeleza wito kuokoa wafugaji na wakulima,” aelezea.

Afisa huyo mkuu mtendaji wa apu hiyo ambaye ni baba wa watoto wawili, ana imani bobbi itasaidia kuangazia changamoto zinazozingira sekta ya kilimo-ufagaji-biashara, hususan kutimua mabroka sokoni.

Wakati wa mahojiano, alifichua kwamba anaendelea na mikakati kuibuka na ukurasa ambao wateja watakuwa wakitoa maoni ya huduma wanazopokea.

“Mpango huo utasaidia kulainisha huduma, na mavetinari na wauzaji kuwajibika.”

Utendakazi wa bobbi unaendelea kupata umaarufu, washirika wakiukumbatia.

“Nikiwa vetinari na mtoaji huduma za mifugo, apu ya bobbi ndiyo afisi yangu,” adokeza James Mwangi, afisa binafsi aliyesajiliwa na idara husika ya mifugo nchini ambaye hutoa huduma katika Kaunti ya Kiambu na Nairobi.

Mtaalamu Mwangi amekuwa akitoa huduma za mifugo zaidi ya miaka saba.

  • Tags

You can share this post!

Msikubali kutishwa na UDA, Uhuru aambia polisi

Kimemia ateua kamati kukagua miradi ya kaunti

T L