Makala

AUNTY POLLY: Fafanua, hedhi huwa nyekundu kila mara

April 16th, 2019 1 min read

Na PAULINE ONGAJI

MARA kwa mara hasa siku kadha baada ya hedhi yangu kuanza, rangi hubadilika na kuwa nyekundu hafifu. Ningependa kujua iwapo damu ya hedhi huwa nyekundu kila mara?

Karyn, 16, Mombasa

Tafiti kadha za masuala ya afya ya uzazi zinaonyesha kuwa sio lazima damu ya hedhi kuwa nyekundu kila mara. Ni kawaida kwa damu ya hedhi kuwa ya rangi ya hudhurungi vilevile nyekundu. Damu inayovuja huwa tofauti kila wakati unapokumbwa na hedhi. Damu yaweza kuanza kwa kuwa nyekundu hafifu kisha kubadilika na kuwa nyekundu thabiti siku za kati kati, na mwishowe hudhurungi, hedhi inapokaribia kuisha. Wasichana wengi hukumbwa na wasiwasi iwapo hedhi yao ni ya kawaida. Hata hivyo, ili kuondoa wasi wasi huo na kukabiliana na tatizo iwapo lipo ni vyema kuzungumza na daktari au mhudumu wa afya.

 

Babangu amekuwa akinichapa sana na naanza kuhisi kana kwamba napaswa kumuitia polisi. Kwa kutumia mshipi amekuwa akinichapa miguuni, mikononi na mgongoni, suala ambalo limekuwa likiacha majeraha mwilini mwangu. Nahisi kutoroka nyumbani. Nifanyeje?

Elias, 18, Nairobi

Shukrani sana kwa kuzungumzia suala hili badala ya kunyamaza. Lakini mwanzo ningependa kujua ni nini hasa humchochea babako kukuchapa? Je, anatumia vileo au mihadarati au kuna jambo unalofanya asilopenda? Mbali na hayo, kulingana na jamii na dini nyingi, adhabu ni sehemu ya malezi. Katika jamii za Kiafrika kuna baadhi ya wazazi wanaoamini sana mbinu kali za adhabu na huenda anadhani kuwa anakutia adabu. Lakini bila shaka adhabu hii imevuka mpaka na haupaswi kunyamazia suala hili. Zungumza na babako, na kama ni ngumu, husisha mtu yeyote mkomavu uliye na uhusiano wa karibu naye. Yaweza kuwa mamako, mwalimu, jamaa au hata mshauri nasaha shuleni.