Makala

AUNTY POLLY…: Nahofia huenda nikarajelea ulevi

May 7th, 2019 1 min read

Na PAULINE ONGAJI

KWA wiki kadha sasa nimekuwa nikikumbwa na tamaa ya kunywa pombe. Tatizo ni kwamba mwaka jana nilikuwa nimetawaliwa na pombe kiasi cha kuwa singeweza kufanya chochote pasipo kulewa. Kutokana na sababu hii, nahofia kwamba endapo nitarejelea pombe tena, basi huenda ikanitawala kwa mara nyingine. Nifanyeje?

Jacintah, 23, Nairobi

Kwanza kabisa hongera kwa kukiri kwamba una tatizo. Sio watu wengi wanaozungumzia kwa uwazi kila wanapokumbwa na matatizo ya aina hii. Pia, ningependa kukumbusha kwamba, japo uliwahi kutawaliwa na pombe, muda huu wote umekaa soba ni ishara kwamba unazidi kupata nguvu za kukabiliana na kiu ya vileo. Kuna mbinu kadha zinazosaidia watu wanaojaribu kujikomboa kutokana na matumizi ya vileo au aina nyingine ya mihadarati. Kwanza kabisa waweza kujihusisha na mambo mengine ambayo yataondoa mawazo yako kutoka hisia za kutaka kutumia kileo. Kwa mfano spoti, kusikiza muziki au hata kusafiri. Vile vile ikiwa kuna mtu au kitu kinacholeta kumbukumbu ya matumizi haya, basi kiondoe maishani mwako.

 

Nasoma katika shule ya upili ya mseto. Darasani mwetu nimegundua kwamba kuna marafiki zangu wanaojihusisha na mahusiano yasiyofaa na hata kuna fununu kwamba kuna wale ambao tayari wameanza kujihusisha na tendo la ndoa. Najua wanachofanya ni kibaya lakini wao ni marafiki zangu, na hivyo siwezi wakemea. Naomba ushauri.

Javan, 17, Mombasa

Inatia matumaini kwamba unajua kwamba wanachofanya ni makosa. Pia, ningependa kukuambia kwamba ni vigumu kutembea na wezi na uepuke kuwa mwizi. Kwa kusema hivi namaanisha kwamba ni rahisi kwa hao marafiki zako kukushawishi ujihusishe na tabia zao iwapo utazidi kujimuika nao. Kabla ya kujitenga nao, jaribu kuwakosoa. Ikiwa hawatakusikia, basi hauna budi ila kuachana nao kabisa. Hatua ya kwanza ya kutengana nao ni kuanza kufanya mambo tofauti kama vile kwenda darasani peke yako, kutojumuika nao wakati wa chakula, vilevile kukaa mbali nao darasani.