Makala

AUNTY POLLY: Niko kidato cha tatu na sijapata hedhi

July 2nd, 2019 1 min read

Na PAULINE ONGAJI

NIKO katika kidato cha tatu na sijaanza kupata hedhi ilhali wenzangu wananiambia kwamba wao walianza wakiwa katika shule za msingi. Mbali na hayo, kwa miezi kadha sasa nimekuwa nikitokwa na maji ukeni. Ningependa ushauri wa kiafya kuhusu suala hili.

Jacinta, 17, Mombasa

Kulingana na wataalamu, kuna baadhi ya wasichana ambao hushuhudia hedhi mapema, ilhali wengine hufanya hivyo wakiwa wamechelewa kidogo. Kwa hivyo ni kawaida. Aidha wanasema kwamba katika kipindi cha kati ya miezi sita na mwaka mmoja kabla ya msichana kuanza kushuhudia hedhi yake ya kwanza, mwili wake huanza kutoa maji maji katika sehemu ya uke. Hii husababishwa na mabadiliko ya viwango vya homoni mwilini. Majimaji haya husaidia kusafisha sehemu ya uke. Hata hivyo, ni vyema kutambua tofauti ya majimaji haya yakilinganishwa na mengine.Majimaji haya huwa mepesi na meupe au krimu na hutoa harufu kidogo. Endapo utashuhudia ya manjano na yenye harufu mbaya huku yakisababisha mwasho, basi ni wakati wa kumuona daktari. Hii yaweza kuwa kutokana na maradhi. Ndiposa unashauriwa kuhakikisha kwamba unatafuta ushauri wa kimatibabu kila unapoanza kushuhudia hali isiyo ya kawaida katika sehemu hii.

 

Utajuaje iwapo tarehe ya mwisho ya kutumika kwa tembe za uzazi imetimia?

Maula, 21, Mombasa

Lazima kila bidhaa iwe imebandikwa tarehe ya kuundwa na tarehe ya kuharibika. Mbali na hayo, kuna mambo kadha ambayo yaweza kusababisha tembe hizi hii kuharibika hata kabla ya tarehe ya mwisho kwa mfano uhifadhi duni. Isitoshe, unapaswa kuwa mwangalifu unaponunua bidhaa kama dawa na uhakikishe kwamba unazipata kutoka duka au hospitali halali na iliyoidhinishwa.