Makala

AUNTY POLLY: Nitajuaje hana ugonjwa wa zinaa?

March 26th, 2019 1 min read

Na PAULINE ONGAJI

NINA mpenzi niliyekutana naye miezi kadha iliyopita. Amenizidi umri na ana tajriba ya masuala ya mahaba kwani yeye mwenyewe aliwahi nifichulia kwamba zamani alikuwa na wapenzi wengi kabla ya kubadili tabia. Sasa ananisukuma tushiriki tendo la ndoa lakini ninahisi kana kwamba bado siko tayari. Isitoshe, hatufajafanyiwa uchunguzi wa kimatibabu kubaini iwapo hatuna maradhi ya zinaa na amekuwa akikwepa kila ninapojaribu kuzungumzia suala hili. Je, kuna ishara ambazo unapaswa kuangalia kujua iwapo mtu ameambukizwa maradhi ya zinaa?

Genna, 19, Mombasa

Pongezi kwa kuonyesha wasiwasi kuhusu suala hilo. Hii ni ishara ya ukomavu. Ni kawaida kukumbwa na hofu hasa ikiwa unazungumzia suala hili kwa mara ya kwanza. Pia, ningependa kukujulisha kwamba ni vigumu sana kutambua ishara za maradhi ya zinaa tu kwa kumwangalia mtu. Hii ni hasa ikizingatiwa kuwa ni vigumu pia kwa mgonjwa anayeugua kutambua anaugua kabla ya kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu. Aidha, unapaswa kujua kwamba hili halipaswi kuwa jambo la kulazimishwa. Ikiwa mwenzio anakupenda na anakujali hatakuwa na tatizo lolote ukizugumza naye kuhusu suala hili. Suala la kushiriki mahaba linapaswa kuwa la hiari na iwapo unahisi kana kwamba una tashwishi, basi usifanye hivyo. Aidha, hii huwa hatua kubwa maishani na haupaswi kulazimishwa. Unapaswa kuwa tayari kufanya hivyo pasipo kusukumwa. Mbali na hayo unapaswa kufahamu kwamba kuna hatari ya kuambukizwa maradhi ya zinaa, kushika mimba, au vyote viwili, suala ambalo laweza kubadilisha maisha yako. Lakini kama wasemavyo, mgala muue na haki mpe. Ikiwa mwenzako amekueleza ukweli kuhusu mahusiano yake ya awali, hiyo ni ishara kwamba atakuwa muwazi ukimzungumzia kuhusu hatari zinazotokana na kushiriki tendo la ndoa. Ikiwa mnahisi kwamba nyote mko tayari kuchukua hatua hii, basi nendeni katika kituo cha afya kupimwa pamoja au kuhakikisha kuwa unatumia vyema kinga kila mara.