Makala

AUNTY POLLY: Rafiki anidhalilisha mtandaoni, nisaidie

February 19th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

Kwa muda sasa nimekuwa nikidhulumiwa na kutukanwa kila mara hasa mtandaoni na mmojawapo wa marafiki zangu wa zamani. Tatizo ni kwamba nimemhusisha mwalimu mkuu na hata mzazi wa msichana huyu, lakini ni mimi ninayelekezewa kidole cha lawama. Kwa upande wangu, wazazi wangu hawachukui hatua yoyote ninapowazungumzia. Nifanyeje?

Lisa, 16, Nairobi

Kwanza kabisa nakupongeza kwa kujitokeza na kuzungumzia suala la undani kama hili. Ninajua kwamba inauma kupitia tatizo la aina hii hasa ikiwa huna wa kumwendea na kumwelezea. Ikiwa unahisi kwamba wazazi wako hawajachukua hatua yoyote kukulinda kutokana na matukio haya, unaweza jaribu kuzungumza na mtu yeyote mkomavu ambaye ataelewa hali yako; mtu ambaye una uhusiano wa karibu naye. Yaweza kuwa mwalimu, jamaa au mshauri nasaha shuleni. Zaidi ya yote unapaswa kuelewa kwamba huna makosa na hivyo hupaswi kujilaumu. Ili kukabiliana na mihemko unaweza jihusisha na mambo mengine ambayo kidogo yataelekeza mawazo yako kwingineko. Kwa mfano kuandika jarida la kueleza hisia zako, kusikiza muziki, kutazama filamu, kujihusisha na spoti au kujumuika na watu wengine. Mbali na hayo litakuwa jambo la busara iwapo utapunguza uwepo wako mtandaoni.

Kwa wiki kadha sasa nimekuwa nikihisi kana kwamba nataka kukaa peke yangu. Licha ya kuwa nina marafiki zangu nimekuwa nikihisi mpweke kwani nahisi kana kwamba nikiwasongea nawakasirisha kila ninapofungua kinywa. Nitafanyeje ili nirejeshe furaha niliyokuwa nayo miaka ya zamani.

Felicia, 13, Mombasa

Shukran kwa kujitokeza kuzungumzia suala hili. Kwanza kabisa ningependa kujua nini kinachokufanya uhisi kana kwamba unawakasirisha marafiki zako kila unapofungua kinywa? Je wao hukuambia? Umewahi zungumza na marafiki zako kuhusiana na hisia zako, na je jibu lipi ambalo wamekuwa wakikupa? Pili, ningependa kukufahamisha kwamba marafiki wa kweli hawapaswi kukufanya uhisi kana kwamba uko jela. Ukiwa nao unapaswa kuwa huru, na ikiwa hauhisi hivyo basi wakati wa kujitenga nao umetimu. Zaidi ya yote unapaswa kuelewa kwamba upendo halisi unapaswa kutoka ndani yako. Jipende kwanza kabla ya kufurahishwa na mambo yanayokuzingira. Rudisha nyuma mawazo yako na ufikirie mambo yaliyokuwa yakikufurahisha zamani na ujaribu kuyarudia.