Makala

AUNTY POLLY…: Rafiki yangu ana matatizo ya kula

May 21st, 2019 1 min read

Na PAULINE ONGAJI

NIKO katika kidato cha tatu katika shule moja jijini Nairobi. Nina rafiki yangu ambaye nimegundua kwamba ana matatizo ya kula. Kwa mfano tukiwa kwenye ukumbi wa maankuli mchana, hali. Wakati mwingine anakula kupita kiasi. Tabia hii ni ya kawaida au napaswa kumsaidia kupata ushauri wa kimatibabu?

Nelima, 18, Nairobi

Sio watu wengi wanaotambua wanapokumbwa na tatizo la kula. Shida hii huwakumba wasichana kwa wavulana. Kulingana na wataalamu wa kiafya, matatizo haya yanaweza kutokana na mchanganyiko wa shida za kimwili na kimawazo. Yeyote anayekumbwa na hali hii anahitaji usaidizi wa kitaalamu ili arejee katika hali yake ya kawaida ya kula. Sio kawaida kwa watu wanaokumbwa na hali hii kulizungumzia hadharani na hivyo anza kwa kumfahamisha mwenzio kwamba anakumbwa na tatizo la kiafya. Kwa upande wake, lazima awe tayari kuzungumzia suala hili. Ikiwa yuko tayari mfanye atulie kwa kumsikiza bila kuonekana kana kwamba unamhukumu. Aidha, unapaswa kukumbuka kuwa sio rahisi kurejelea hali ya kawaida kwani hii huchukua muda. Inapowadia katika suala hili, unapaswa kuwa mpole na kumwelekeza taratibu. Pia, nina uhakika kuwa hauna utaalamu unaohitajika kumsaidia, na hivyo sharti mshauri nasaha ahusishwe hapa.

 

Chakula kinachouzwa katika mkahawa wa chuo chetu sio lishe bora na hivyo ningependa kujua ni mlo upi sahili naweza kuandaa na kubeba kutoka nyumbani?

Bernice, 22, Mombasa

Kuna mambo kadha ambayo unapaswa kuzingatia unapoandaa chakula cha kubeba kutoka nyumbani. Jumuisha nafaka ambazo hazijakobolewa, protini iliyo na kiwango cha chini cha mafuta, matunda na mboga. Pia, unapaswa kuzingatia chakula kisicho na supu ili kuzuia isimwagike na kukuchafua. Aidha, unapaswa kuhakikisha kwamba chakula chako kinajumuisha vikundi vyote vya vyakula muhimu. Mfano mzuri wa mlo ni sandwichi, silesi ya nyama, mboga, na saladi. Chochote utakachochagua kinapaswa kujumuisha angalau vikundi vitatu vya chakula na ladha tofauti.