Makala

AUNTY POLLY: Uzani kupitiliza wanitia kiwewe

June 11th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

KWA miezi sasa nimegundua kwamba nimekuwa nikiongeza uzani, suala ambalo linazidi kuathiri umbo langu la kupendeza na kunipa wasiwasi kiasi kwamba nimeanza kujitenga na watu wengine. Kwa nini?

Janey, 18, Nairobi

Ni kawaida kwa watu kuthamini hicho kitu kinachowafanya kuvutia machoni mwa watu wengine. Kwako kitu hicho ni hilo umbo la kupendeza. Lakini ningependa kukuambia kwamba unapaswa kujua kuwa kuna mambo mengi muhimu kukuhusu zaidi ya mwonekano wako.

Pindi unapoelewa hili, basi masuala kama haya hayatakukosesha usingizi.

Haifai kila mara kuwa na wasiwasi kuhusu mwonekano wako. Siku hizi watu wengi wanazingatia sana kuhusu sura nzuri au umbo la kupendeza.

Bila shaka urembo au utanashati utakufanya uwe mvuto kwa wengine, lakini kuna mambo mengine zaidi ya hayo. Japo sio kosa kutaka kuonekana maridadi, kuna mambo mengine muhimu yanayoakisi nafasi yako machoni mwa wengine. Kwa hivyo zingatia kuimarisha mambo ambayo yatadumu hata baada ya sura kunyauka na mwili kupoteza umbo.

 

Nina rafiki yangu tokea utotoni ambaye katika siku za hivi majuzi nimegundua kwamba amekuwa akivuta bangi. Je, nitasamsaidia vipi aachane na uraibu huu?

Jason, 17, Mombasa

Kwanza kabisa hongera kwa kuwa rafiki mzuri. Ningependa kukushauri kwamba hatua ya kwanza ya kumsaidia mwenzako ni kumfanya ajue kwamba umegundua siri yake na nia yako kumsaidia.

Usithubutu kumsengenya, na badala yake mfahamishe wasiwasi wako kuhusu tabia yake. Waweza zungumza na mtu mkomavu mwenye uhusiano wa karibu naye na unayemuamini, pasipo kuwepo kwa hatari ya kumweka mashakani.

Pia, waweza kumhimiza kupata ushauri nasaha.

Mbali na hayo, je, wajua kwamba uraibu wa aina hii mara nyingi huwa kutokana na uvivu au ulegevu. Kwa hivyo, jaribu kumshirikisha katika shughuli zingine zitakazoondoa mawazo yake katika uraibu huu kama vile kusikiza muziki au kujihusisha na spoti.

Na iwapo unahisi kana kwamba kujihusisha kwako katika harakati za kumsaidia kusnahatarisha maisha yako au yake, basi ni wakati wa kujitenga kidogo na kuachia nafasi wataalamu.