Makala

AUNTY POLLY…: Yawezekana kushika mimba na umejikinga?

March 19th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

RAFIKI yangu ana mimba licha ya kutumia mbinu za kupanga uzazi. Inawezekana kushika mimba hata iwapo unatumia mbinu za kupanga uzazi?

Marielle, 18, Nairobi

Bila shaka kuna mbinu tofauti za upangaji uzazi lakini ukweli ni kwamba hazikukingi asilimia mia moja. Hii inamaanisha kwamba kuna uwezekano wa kushika mimba hata ikiwa unatumia mbinu ya upangaji uzazi. Hii ndiyo sababu unashauriwa kupata mawaidha ya kitaalamu kabla ya kutumia mbinu yoyote. Tatizo ni kwamba wasichana wengi hufanya kosa la kutumia mbinu fulani ya kupanga uzazi eti kwa sababu inawafaa wenzao. Wajua unapotembelea kliniki ya uzazi kuna masuala mengi watazingatia kabla ya kukushauri kutumia mbinu yoyote ile. Kwa mfano utafanyiwa uchunguzi wa kiafya kubaini iwapo mbinu unayotaka kutumia itaambatana homoni mwilini mwako. Kando na hayo unapaswa kukumbuka kwamba mbinu zinazohusisha kumeza tembe, kudungwa sindano au kuingizwa vifaa fulani mwilini, kamwe hazikuepushi na maambukizi ya zinaa. Kando na hayo, kiumri ungali mchanga na itakuwa vyema iwapo utapunguza kasi ya kushiriki ngono.

Kwa miezi minne sasa nimekuwa katika uhusiano na kaka huyu ambaye mwanzoni alionekana mzuri. Lakini muda ulivyosonga alianza kuonyesha tabia za kushangaza ikiwa ni pamoja na kunisukuma tushiriki ngono. Nina wasiwasi kiasi kwamba sijui iwapo fungamano hili lanifaa. Nitajua vipi kwamba niko katika uhusiano mzuri?

Jasmine, 16, Nairobi

Kwanza kabisa hongera kwa kuonyesha ukomavu licha ya umri wako mdogo. Hii ni kwa sababu ni vigumu hasa katika umri mdogo kwa mtu kuwa na tashwishi kuhusu uhusiano aliomo. Lakini, kuna ishara ambazo zitakuwa mwongozo kwako ili kutambua ikiwa uhusiano ulio nao ni mzuri. Ishara kuu anakupenda ni kwamba lazima akuheshimu. Heshima inamaanisha kwamba awe tayari kukubaliana na uamuzi wako hasa ikiwa unahusisha mwili wako. Kwa sasa ungali mchanga na huo wasiwasi ni ishara tosha kwamba haupaswi kufanya hivyo. Pia unapaswa kujua kwamba haujahitimu umri unaomruhusu yeyote kisheria kushiriki nawe mahaba. Mweleze na iwapo hayuko tayari kuelewa, achana naye. Ikiwa amezidi miaka 18 na hataki kukusikiza, mkumbushe kwamba anaenda kinyume na sheria na anaweza chukuliwa hatua.