Makala

AUNTY POLLY: Yawezekana nina ugonjwa wa zinaa?

June 25th, 2019 1 min read

Na PAULINE ONGAJI

HUYU wa mwanzo leo anauliza hivi:

Nina umri wa miaka 22 na kwa miezi miwili sasa nimekuwa na mpenzi ambapo tayari kwa mara kadha tumeshiriki tendo lenyewe la wapenzi bila kutumia kinga. Sio kwamba simuamini lakini nimekuwa nikihisi mgonjwa kimwili suala ambalo limenifanya kushuku kuwa huenda nimeambukizwa maradhi ya zinaa. Naomba ushauri.

Katrina, 22, Mombasa

Kabla ya kukupa ushauri wowote ningependa kukuuliza iwapo wewe na mwenzako mlipimwa kiafya kabla ya kuchukua hatua hii. Ningependa kukukumbusha kwamba kushiriki tendo hilo bila kinga hasa ikiwa nyote hamjapimwa kubaini iwapo mna maradhi ya zinaa, kunawaweka nyote katika hatari ya maambukizi. Hata hivyo, tayari mshashiriki kitendo hiki na lawama hazitasaidia. Ili kubaini iwapo umeambukizwa au la, njia pekee ni kupimwa. Itakuwa vyema iwapo nyote mtaenda hospitalini kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu na mpate tiba iwapo kuna maambukizi yoyote. Nyote mwaweza tembelea kituo cha kiafya cha serikali ambapo mtapata ushauri kuhusu masuala ya uzazi bila malipo.

 

Mimi ni mvulana wa shule ya upili. Kwa wiki kadha nimeshuhudia uvimbe fulani mdogo ambao umechipuka kwenye titi langu la kushoto. Mwanzoni niliupuuza lakini baada ya kufanya tafiti kadha mtandaoni, nimegundua kwamba hii yaweza kuwa ishara ya matatizo ya kiafya na hasa kansa ya matiti. Je, ni kawaida kwa wavulana kukumbwa na maradhi haya?

Victor, 17, Nairobi

Naam! Japo kansa ya matiti huwakumba sana wanawake, pia wanaume wanaweza pata maradhi haya. Lakini kabla ya kuanza kujishuku itakuwa vyema kwenda hospitalini ili kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu, kwani ni daktari pekee aliye na ujuzi wa kutosha kukuhakikishia usalama wako kiafya. Aidha, ningependa ufahamu kwamba, wakati mwingine ni kawaida kwa mabadiliko ya aina hii kushuhudiwa miongononi mwa wavulana hasa walio katika umri wa kubalehe. Tembelea kituo cha kiafya kilicho karibu nawe ili ufanyiwe uchunguzi wa kimatibabu.