KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Australia kuvaana na Argentina katika hatua ya 16-bora baada ya kucharaza Denmark kwa 1-0 katika Kundi D

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Australia kuvaana na Argentina katika hatua ya 16-bora baada ya kucharaza Denmark kwa 1-0 katika Kundi D

Na MASHIRIKA

AUSTRALIA walifuzu kwa hatua ya 16-bora ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 16 baada ya kuduwaza Denmark kwa kichapo cha 1-0 katika Kundi D mnamo Jumatano uwanjani Al Janoub.

Mara ya mwisho kwa Australia kuingia raundi ya 16-bora kwenye Kombe la Dunia ni 2006 wakijivunia huduma za Harry Kewell, Tim Cahill na Mark Schwarzer. Walidenguliwa na Italia katika hatua hiyo mwaka huo nchini Ujerumani.

Denmark walioshuka dimbani wakihitaji ushindi, walianza mechi kwa matao ya juu huku wakimiliki asilimia kubwa ya mpira. Hata hivyo, walifungwa bao la kushtukiza baada ya fowadi Mathew Leckie kumwacha hoi kipa Kasper Schmeichel katika dakika ya 60.

Ushindi dhidi ya Denmark ulishuhudia Australia wakimaliza kampeni za Kundi D katika nafasi ya pili kwa alama sita, sawa na Ufaransa waliokomolewa 1-0 na Tunisia katika mechi yao ya mwisho. Hata hivyo, Ufaransa ambao ni mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia walidhibiti kilele kutokana na wingi wa mabao.

Denmark walilazimishwa kufunganya virago nchini Qatar baada ya kuvuta mkia wa Kundi D kwa alama moja pekee kutokana na mechi tatu.

Australia sasa watavaana na Argentina katika hatua ya 16-bora leo Jumamosi, Disemba 3, 2022 ugani Ahmad Bin Ali.

Argentina waliibuka wa kwanza katika Kundi C kwa alama sita baada ya kupepeta Poland 2-0 mnamo Jumatano usiku.

Denmark walianza kampeni za Kombe la Dunia mwaka huu wakipigiwa upatu wa kutamba baada ya kutinga nusu-fainali za Euro 2020 na kuridhisha zaidi kwenye mashindano ya Uefa Nations League kwa kulaza Ufaransa nyumbani na ugenini.

Hata hivyo, walishindwa kuwika nchini Qatar na wanarejea nyumbani baada ya kufunga bao moja pekee kutokana na mechi tatu za Kundi D. Sasa hawajashinda mechi yoyote kati ya sita zilizopita kwenye fainali za Kombe la Dunia. Nne kati ya michuano hiyo ambayo wamepiga imekamilisha kwa sare.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Jubilee sasa haitashiriki maandamano

Ashtakiwa kutukana polisi wa kike wawili

T L