Auza nyumba ya babake akimdai Sh200,000

Auza nyumba ya babake akimdai Sh200,000

Na STEPHEN ODUOR

MWANAMUME katika eneo la Garsen, Kaunti ya Tana River ameshangaza wenyeji kwa kuuza nyumba ya babake akimdai Sh200,000.

Bw Francis Makasi, 35, alikuwa amempa babake pesa hizo kugharamia sherehe ya kitamaduni ya kuchumbiana na mpenzi wake kabla wafunge ndoa.

Sherehe hiyo ilikuwa imepangiwa kufanyika nyumbani kwao Jumamosi, Agosti 7 lakini ikasemekana babake alitumia pesa alizopewa kucheza kamari katika baa iliyo karibu na kwao.

Kulingana na Bw Joseph Masih ambaye ni mjombake Bw Makasi, mzee huyo alikuwa akionekana katika baa akiwaburudisha marafiki wake huku akicheza kamari inayohusiana na michezo ya Olimpiki ambayo inaendelea nchini Japan.

“Amekuwa shabiki wa timu ya kandanda ya Brazil tangu zamani. Mmoja wa marafiki wake aliniambia alipoteza Sh50,000 katika kila mchezo ambao alikuwa anatarajia kushinda. Hasara ya mwisho ilitokea wakati Brazil na Mexico walitoka sare tasa,” akasema.

Yasemekana alipotambua amebaki na Sh25,000 pekee, aliamua kumpa kakake Sh20,000 ili azitumie kwa maandalizi ya sherehe kisha akasafiri hadi mashambani.

Bw Makasi alirudi nyumbani Jumatano iliyopita akitarajia kuendelea na maandalizi lakini akaambiwa babake hakuwepo. Mjombake ndiye alimsimulia matukio hadi jinsi alivyoachiwa Sh20,000.

“Alishtuka sana akaniambia alikuwa amemtumia babake jumla ya Sh200,000 na alitarajia mipango ingekuwa imekaribia kukamilika,” akasema Bw Masih.

Bw Makasi alipompigia simu, babake alimwambia apeleke sherehe hizo mashambani kwa sababu lazima wazee washirikishwe.

Alienda mashambani Ijumaa kukutana na babake akampata mamake wa kambo nyumbani, huku babake akiwa amelewa chakari.

Huku akithibitisha matukio hayo, mama huyo, Bi Hellen Magawa alisema aliamua kumwambia Bw Makasi atafute pesa za kuandaa sherehe hivyo la sivyo angeaibika.

Kulingana naye, wawili hao walibishana asubuhi na baba akamwambia mwanawe kwamba alihitaji kuongeza pesa za maandalizi.

“Alimwambia Sh200,000 zilikuwa chache mno kwa hafla hiyo kwa hivyo alitaka kucheza kamari ili ziongezeka lakini akapoteza,” akaeleza Bi Magawa.

Aliuza nyumba ya babake kwa Sh500,000 kisha akaondoka. Bw Makasi aliambia Taifa Leo ameachia mjombake na wazee watatue suala hilo lakini kwa sasa amefutilia mbali mipango ya sherehe.

You can share this post!

Jiandaeni kwa kiangazi na njaa, shirika laonya

Aliyekuwa meya Lamu ageuka bodaboda kujipatia riziki