Dondoo

Auza suti ya polo apate hela za saluni

July 26th, 2020 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

KERICHO

KIPUSA mtaani hapa aliwashangaza wengi alipoamua kuuza suti mpya ya mumewe ili apate fedha za kumwezesha kwenda saluni kurembeshwa nywele.

Kulingana na mdokezi, kwa siku nyingi kipusa alikuwa akimuomba mumewe hela za kwendea saluni lakini hakuwa akimpa.Inadaiwa polo alikuwa akimkemea mkewe akidai hana fedha za kuharibu ilhali alikuwa akinunua suti mpya kila baada ya mwezi mmoja.

Duru zinasema kwamba kipusa aliamua kuchukua suti moja na kuiuza ili apate pesa za kwenda saluni.

“Baada ya kuuza suti ya mumewe, kipusa alifululiza moja kwa moja hadi saluni akapambwa nywele mtindo aliotamani kwa siku nyingi,” mdaku alisema.

Inasemekana polo aliporejea jioni, alishangaa kumuona mkewe akiwa amebadilika.“Kwani ulitoa wapi pesa ulizotumia kwenda saluni kupambwa nywele zako?” polo alimuuliza mkewe.

Duru zinasema kipusa aliamua kunyamaza jambo lililomkasirisha polo.

“Mbona wajitia hamnazo. Ni nani aliyekupa pesa,” polo alifoka.Inasemekana kwamba mwanadada alimdanganya polo kuwa ni mama yake aliyempa hela lakini jamaa hakuamini ndipo akaenda moja kwa moja hadi katika chumba cha kulala na akakosa moja ya suti zake mpya.“Sioni suti yangu moja.

Imeenda wapi?” alimuuliza mkewe ambaye aliendelea kunyamaza tu, jambo lililomfanya polo kuwaka zaidi.Duru zinasema kipusa alilazimika kupasua mbarika.

“Wewe umezoea kunidhulumu. Ni mara ngapi nimekwambia unipe pesa niende saluni na hutaki kunipa,” kipusa alimshtumu polo. Penyenye zinasema kipusa alipewa kofi moja kali sana.

“Nakupa dakika ishirini uwe umerudisha suti yangu,” polo alimkaripia kipusa.Inadaiwa kipusa alipoona mambo yameharibika, alichomoka mbio huku akiwaacha majirani kwa vicheko.