Habari

Avuna kwa sura kama ya Uhuru

August 14th, 2020 2 min read

Na PETER MBURU

MWANAMUME ambaye amepata umaarufu ghafla kutokana na kufanana na Rais Uhuru Kenyatta, ameanza kuvuna matunda baada ya kuzawidiwa gari Alhamisi.

Michael Njogo Gitonga ambaye picha zake zimekuwa zikisambaa mitandaoni kwa siku kadhaa kwa kuwa na sura kama ya Rais Kenyatta, alipokea gari hilo na kampuni ya uuzaji magari ya Maridady Motors.

Japo kampuni hiyo haikufafanua aina ya gari ambalo ingemzawidi Bw Gitonga, jana asubuhi ilituma picha katika akaunti zake za mitandao ya kijamii, pamoja na picha za Bw Gitonga akiwa ameketi ndani ya gari na akiwa katika jumba la kuuzia magari.

“Wakenya wenzetu, ni gari gani mnapendekeza Uhunye achukue kutoka duka letu la magari?” kampuni hiyo ikauliza mitandaoni, huku swali likiunganishwa na picha za Bw Gitonga.

Bw Gitonga mwenyewe Alhamisi jioni alithibitishia Taifa Leo kuwa alikuwa katika kampuni hiyo wakiendelea na mazungumzo na wakuu wake, japo hakufafanua zaidi kuhusu walichokuwa wakijadili.

“Nimekuwa hapa Maridady Motors tangu asubuhi na bado tunaendelea na mazungumzo. Labda tutamaliza muda wa saa mbili kutoka sasa,” akasema Alhamisi saa kumi na nusu jioni tulipompigia simu.

Taifa Leo ilijaribu kutafuta wakurugenzi wa kampuni hiyo kufahamu aina ya ushirikiano ambao ilikuwa ikipanga kuwa nao na Bw Gitonga na aina ya gari ambalo ilimzawidi.

Pia tulitaka kuthibitisha ikiwa ni kweli walikuwa wamempa kandarasi ya kuwa balozi wao kulingana na uvumi uliokuwepo mitandaoni Alhamisi.

Kutokea kwa Bw Gitonga mbele ya umma kumechochea gumzo tele miongoni mwa Wakenya wakijiuliza iwapo ana uhusiano wowote na Rais Kenyatta, hasa baada ya baadhi ya vyombo vya habari kuchapisha habari zikiangazia maisha yake.

Awali alikuwa amelalamika kuhusu jinsi hali yake ya kimaisha imeharibiwa na kuibuka kwa ugonjwa wa Covid-19 uliomlazimu kufunga kazi yake ya baa: “Covid-19 imeniathiri sana. Nimekuwa nikiomba Mungu amalize janga hili kwani limenisukuma hadi mwisho.”

Atamani kukutana na Rais

Akihojiwa na vituo tofauti vya habari siku chache zilizopita, Bw Gitonga alikiri kuwa amekuwa na ari ya kutaka kukutana na Rais Kenyatta, kutokana na jinsi watu wengi wamekuwa wakimfananisha naye.

“Mimi hata huwa nashangaa na nashindwa nini kilifanyika kati yangu na Uhuru. Tunafanana sana. Mtaani naitwa Uhuru na kila mtu,” akasema.

Akaeleza: “Swali ambalo ninaweza kumuuliza Rais kwanza ni ikiwa yeye ni kakangu.”

Alisema hali hiyo imekuwa ikimsababishia mseto wa matokeo maishani, mara fulani akiepuka mabaya na wakati mwingine kulazimika kuwapa pesa watu wanaomuomba mara kwa mara kwa kuamini kuwa anafaa kuwa nazo; kwani anafanana na Rais.

“Wakiniona tu wanaanza kuniambia ‘Uhunye sijakula’, ‘Uhunye acha kitu’ na inanibidi niwape kidogo nilicho nacho,” Bw Gitonga akasema alipokuwa akihojiwa wiki iliyopita.

Alisema ana watoto watatu, wawili wa kiume na mmoja wa kike, na kuwa nao pia huitwa “watoto wa Uhuru.”

Japo mamake aliaga dunia, bado anatumai kuwa siku moja babake atajitokeza ili atatue fumbo la ikiwa ana uhusiano wowote na Rais.

“Nikiwa nimeketi hapa leo niliwaza na kujiambia afadhali babangu akiwa alipo angejitokeza tu na kuniambia kuwa ndiye aliyenizaa. Nitamshukuru na kumwambia anibariki,” akasema Bw Gitonga alipokuwa akihojiwa majuzi.