Dondoo

Awaka demu kuzidisha bili ya mlo

February 24th, 2020 1 min read

Na LUDOVICK MBOGHOLI

VOI MJINI

POLO mmoja mjini hapa, hakuamini alipolazimishwa kumlipia demu bili kubwa ya mlo.

Inasemekana jamaa alimtongoza kipusa naye akameza chambo na wakaenda kukesha lojing’i.

“Walikunywa pombe kabla ya kwenda kukodisha chumba,” alidokeza mdaku huku ikiarifiwa ilipofika saa mbili asubuhi walienda kupata kiamsha kinywa.

“Waliingia hotelini wakaagiza chai na vitafunio,” asimulia mdokezi huku ikidaiwa demu alikunywa chai taratibu.

Polo alimaliza yake na akaondoka kwenda dukani.

Alipoondoka demu aliagiza pilau ya kuku na maziwa baridi ya kuteremshia.

“Alikula haraka haraka akamaliza, akaagiza afungiwe kuku mzima wa kubanikwa na chips mbili,” alisimulia mdaku wetu.

Alipofungiwa alivyoagiza, alivitia mkobani na akatulia kumsubiri polo ambaye alirejea akiwa na pakiti ya sigara, akakaa karibu naye na kumpapasa mabega.

“Acha nikalipe bili halafu nikupe nauli tuachane,” jamaa alijishasha.

Polo, alipofika kwa keshia hakuamini alipokabidhiwa bili ya zaidi ya Sh2,300.

“Hapana, fanyeni tena hiyo hesabu,” jamaa aliteta huku akimkodolea macho demu. Jamaa alielezwa kilichofanya bili kuwa kubwa na akashtuka.

“Mwenzako amekula pilau na kuku kisha akafungiwa mnofu mwingine na chipsi. Hesabu yetu iko sawa na kama uko na maswali, muulize mtu wako,” keshia alimweleza.

Jamaa alijaribu kuzusha lakini akalemewa wahudumu walipoingilia kati.

“Jamaa alipokuwa akichemka kwa hasira, demu alikuwa ametulia na kumtazama tu,” alieleza mdokezi.

Inasemekana jamaa alijishika kichwa na kwa kuwa hakuwa na pesa zaidi, ilibidi afulize kwa M-pesa akalipa bili.

“Alilipa na na kuondoka bila kumuaga demu ambaye pia aliondoka kivyake,” alieleza mdokezi.