Habari Mseto

Awamu ya kwanza ugavi wa chakula kwa familia za kipato cha chini Mombasa kukamilika kesho Jumanne

May 18th, 2020 2 min read

Na MISHI GONGO

AWAMU ya kwanza ya ugavi wa chakula kwa familia za kipato cha chini katika Kaunti ya Mombasa unatarajiwa kukamilika Jumanne.

Uzinduzi wa awamu hiyo ulifanyika wiki tatu zilizopita na tayari mpango huo umetekelezwa katika baadhi ya maeneo yakiwemo Jomvu na Nyali.

Hapo kesho ugavu utakuwa katika maeneo bunge ya Kisauni na Likoni ambayo ndiyo yatafanikisha awamu ya kwanza.

Kulingana na Mwenyekiti wa Shirika la Msalaba Mwekundu Bw Mahmoud Noor, awamu ya kwanza ya mradi huo ililenga familia 50,000 lakini kufikia sasa wamezifikia familia 35,000

“Tunalenga familia 237,000 katika Kaunti ya Mombasa. Ugavi wa chakula umegawanywa katika awamu mbili ambapo awamu ya kwanza inalenga familia 50,000 huku awamu ya pili ikikusudiwa itakamilisha mpango katika familia zilizosalia,” akasema Bw Noor.

Katika mradi huo familia zilizoandikishwa zinapokea maharagwe, mchele, mafuta ya kupikia, unga wa ugali na ule wa ngano pamoja na sodo kwa wanawake.

Mwenyekiti huyo alisema awamu ya pili itaanza baada ya wiki moja.

Alisema mpango huo unakumbwa na changamoto nyingi ambazo wanaendelea kuzitatua.

 

Mwenyekiti wa Shirika la Msalaba Mwekundu Mahmoud Noor (mwenye jaketi jekundu) pamoja na maafisa kadhaa wa Kaunti ya Mombasa wakikagua chakula cha msaada. Picha/ Hisani

Alisema kwamba baadhi ya watu waliotwikwa jukumu la kuzisajili familia hizo waliitekeleza shughuli hiyo kwa upendeleo hali ambayo imechangia kucheleweshwa kwa ugavi jinsi ilivyoratibiwa.

“Baadhi ya watu tuliowatwika jukumu la kugawa chakula, walifanya ubaguzi. Kuna wale waliosajili jamaa zao na wale walioandikisha watu wawili kutoka familia moja,” akasema Bw Noor.

Hata hivyo, alisema visa vya mapendeleo vilikuwa vichache, akisisitiza kuwa ni familia zisizojiweza tu ndizo zilizonufaika na mradi huo wa chakula.

Hata hivyo, Bw Noor alisema idadi ya familia walizozilenga inaweza ikaongezeka kufuatia Wakenya wengi kupoteza kazi ndani ya miezi mitatu iliyopita kutokana na kuingia kwa ugonjwa wa Covid-19.

“Kuna watu walikuwa wanajiweza, lakini kufuatia kampuni nyingi kupunguza wafanyakazi, wengi wameachwa bila ajira hivyo kuongeza idadi ya wasiojiweza,” akasema.

Alisema kuwa serikali haitaweza kusaidia kila mtu, hivyo aliwaomba wahisani kujitokeza kwa wingi.

“Watu wengi wanaumia kutokana na hali mbaya ya uchumi,” akasema.

Aidha alisema wamewapa wakazi wa Mji wa Kale kipaumbele katika ugavi wa chakula kufuatia serikali kuweka marufuko yanayowazuia wakazi kutoka au wengine kuingia eneo hilo kama njia ya kudhibiti virusi vya corona.