Makala

AWAMU YA PILI YA SGR: Wakazi walalamikia athari za mradi Kajiado

June 11th, 2018 2 min read

Na CHARLES WASONGA

KUNDI la wakazi wa Kaunti ya Kajiado limewasilisha malalamishi katika bunge la Seneti wakitaka ujenzi wa awamu ya pili ya mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) usitishwe hadi pale mwanakandarasi atakaposhughulikia athari mradi huo kwa mazingira.

Wakiongozwa na seneta wa zamani wa kaunti hiyo Peter Mositet, wakazi hao wamesema kuwa shughuli ya ujenzi wa reli hiyo kutoka Nairobi hadi Naivasha umesababisha uchafuzi wa maji na hewa huku binadamu, wanyama, na mimea ikiathiriwa pakubwa.

“Mito na vidimbwi vya maji vimechafuliwa na kemikali ambayo hutumia kurahisisha upasuaji wa mawe hali inayohatarisha maisha ya binadamu na wanyama ambao hutegemea maji hayo,” mhandisi Mositet aliambia Kamati ya Seneti kuhusu Ardhi katika majengo ya bunge, Nairobi.

Kamati hiyo inaongozwa na Seneta wa Nyandarua Bw Mwangi Githiomi.

Bw Mositet aliongeza kusema kwamba barabara na majengo yameharibika karibu na matimbo kutokana na mtikisiko unaosababishwa na mitambo ya kubomoa mawe ndani ya matimbo hayo.

Shughuli hizi pia zimesababisha uchafuzi wa hewa katika maeneo ya Enkusero, Sampu, Kibiko Kisamis na katika shamba la Ngong’ Veterinary.

“Kwa hivyo tunaika kamati hii ya seneti kuamuru Shirika la Reli Nchini (KR) na Kampuni ya China Roads and Bridges Corporation (CRBC) kuwajengea wakazi mabwawa ya maji safi kama njia ya kuwasaidia wananchi wanaoteseka.

“Vile vile, tunaitaka seneti kuamrisha kampuni hizi mbili zikarabati barabara na shule ambazo zimeharibiwa katika maeneo ya Ongata Rongai, Kiserian na Ngong,” wakazi hao wanasema kwenye hati yenye malalamishi yao waliowasilisha kwa kamati hiyo.

 

Fidia

Naye Bw Samuel W’ Njuguna ambaye ni mkazi wa Ngong’ alilalamika kuwa ujenzi huo ulianza kabla ya wakazi kulipwa fidia kando na maoni yao kukusanywa kama inayohitajika kulingana na Katiba.

“Kipengee cha 69 cha katiba kinasema wazi kuwa kabla ya mradi wowote kutekelezwa uchunguzi wa madhara yake kwa mazingira unafaa kufanywa na ripoti kuwasilishwa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA. Na wananchi wanafaa kuhusishwa kabla ya mradi wenye madhara kwa mazingira kutekelezwa, hitaji ambalo mwanakandara na shirika la reli hawakuzingatia,” akasema Bw Njuguna.

Seneta Githiomi alitaja malalamishi ya wakazi hao kama yenye “uzito mkubwa” na kuahidi kuwa kamati yake itayashughulikia kulingana na sheria za bunge hilo.

“Malalamishi yameibua masuala yenye mantiki na uzito mkubwa. Kwa hivyo, tutawaita wahusika wengine kama vile Shirika la Reli na kampuni ya CRBC ili kusikiza utetezi wao. Baadaye tutawaita tena kwa mahojiano ya kina kabla ya kuandaa ripoti ambayo tutawasilisha katika kikao cha bunge lote la seneti,” Bw Githiomi akasema.

Naye Seneta George Khaniri aliwahikikishia wakazi hao kuwa wajibu mkuu wa bunge hilo ni kutetea masilahi ya wananchi kama wao.

“Kwa hivyo, muwe na matumaini kuwa tatizo lenu litashughulikiwa ipasavyo kwa manufaa yenu nyote. Mradi kama huu unapaswa kuwanufaisha bali sio kuwasababishia madhila,’ akasema.