Habari Mseto

AWINO: Halmashauri ya Chakula ilileta hasara, heri hizi juhudi za Munya

October 22nd, 2020 2 min read

Na AG AWINO

WASWAHILI husema kata pua uunde wajihi, yaani hakuna uzuri unaokuja bila kupitia machungu fulani.

Hata hivyo, mabadiliko yaliyonuiwa wakati Halmashauri ya Chakula (AFA) ilipobuniwa miaka saba iliyopita hayakupatikana licha ya machungu yaliyotokana na kubuniwa kwake. Kwa miaka saba, sekta ya kilimo imekuwa ikikabiliana na matokea ya uamuzi wa kubuniwa kwa AFA.

Mnamo 2014, chini ya aliyekuwa Waziri wa Kilimo kwa wakati huo Felix Kosgei, mswada wa kubuniwa kwa AFA ulipitishwa bungeni. Ingawa ishara za matatatizo ya kubuniwa kwa AFA ulianza kuonekana mapema, mawaziri waliofuata: Willy Bett na Mwangi Kiunjuri hawakuona hitilafu iliyokuwepo na wala hawakupendekeza kuvunjiliwa kwa AFA. Ndiyo sababu namshukuru Waziri wa sasa wa Kilimo Peter Munya kwa kuleta bungeni miswada mitano ambayo inapendekeza kuundwa upya kwa bodi mbalimbali za usimamizi kama ilivyokuwa zamani japo kwa tofauti kidogo.

Kulingana na miswada ya Munya, kutakuwa na bodi tano ambazo zitasimamia miwa, kahawa, pareto, miraa, mahindi na kadhalika. Tofauti na zamani ambapo kulikuwa na bodi 11, baada ya miswada kupitishwa, kutakuwa na bodi tano ambazo zitagawanywa kwenye vikundi vya kahawa, miraa, vyakula vinavyoliwa na mimea ya kiviwanda kama vile pareto.

Inafaa iwekwe sheria ambayo inaadhibu wafanyakazi wa serikali ambao wanapendekeza mageuzi ambayo hatimaye husababisha hasara. Licha ya kwamba Bw Munya alisema kwamba hawakupoteza pesa kutokana na kubuniwa kwa AFA, kwamba bajeti kila mwaka haikupungua ni ishara kwamba uamuzi wa kuundwa kwa AFA haukufikiriwa vyema.

Bodi zilizovunjwa na kuwekwa chini ya AFA zilikuwa zikisimamia mimea tofauti na hivyo ikawa rahisi kutetea mikakati na kupigania kila maendeleo ya mimea hii.

Kubuniwa kwa AFA ni mfano mwafaka wa namna ukiritimba unavyoweza kuzorotesha sekta ya kilimo. Kwanza, wakurugenzi wakuu wa bodi zilizowekwa chini ya AFA hawakupewa mkataba wa kudumu huku walio chini yao wakiwa na mkataba kamili. Ubunifu na uhuru wa kuimarisha mimea mbalimbali ulisitishwa. Katika maonyesho ya kilimo ya kila mwaka, kibao ambacho kimekuwa kikionekana ni cha AFA na wala siyo bodi zilizokuwa chini yake. Hii iliua nafasi ya bodi hizi katika soko kwani hazikuwa tena na nafasi ya kung’aa na kuuza bidhaa zao kama ilivyokuwa zamani. Yaani AFA iligeuka kuwa muuzaji, mtengenezaji na mtangazaji wa bidhaa zilizokuwa chini yake badala za kuzipa bodi nafasi za kung’aa.

Natumai kwamba wabunge watapitisha haraka miswada ya Munya ya kubuniwa tena kwa bodi mbalimbali za kilimo ili tupate wataalamu katika kila sekta hii ambao wataendesha ipasavyo shughuli za kuinua kilimo nchini. Mfumo wa majaribio bila mtazamo wa kitaalamu ukome kabisa.

Bw Awino ni mwanamawasiliano mwenye ujuzi katika masuala ya Kilimo

[email protected]