Makala

AWINO: Konokono Mwea wasipuuzwe kama gugumaji Victoria

September 10th, 2020 2 min read

Na AG AWINO

GUGUMAJI lilipovamia Ziwa Victoria miaka michache iliyopita, wengi walidhani lilikuwa wingu la kupita.

Lilianza kama ua maridadi ambalo lilikuwa likielea majini kutoka sehemu moja hadi nyingine. Baada ya muda, madhara yake yakaanza kuonekana.

Ikawa vigumu kwa merikebu, madau na mashua, kuanza au kuhitimisha safari zao ziwani. Licha ya juhudi kubwa za serikali kuu na ile ya kaunti kupambana na gugu hili, hakuna ufanisi wowote umeafikiwa. Kufikia sasa, kiasi kikubwa cha pesa kimetumika kuangamiza gugu hili.

Ndivyo hali ilivyo kwa sasa katika eneo la mradi wa mpunga Mwea. Kwa zaidi ya miezi saba sasa, kumekuwa na ripoti kuhusu konokono wageni almaarufu ‘golden apple’ ambao sasa wanatishia uzalishaji wa zao hilo. Wadudu hao wenye asili katika bara la Asia hupenda mchele.

Sasa imekuwa kilio kwa wakulima katika eneo hili ambao wanahofia kwamba hali itazidi kuwa mbaya iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa kupambana nao mapema. Wataalamu wameonya kwamba, konokono hawa ni tofauti na konokono wa kawaida kwani wanapoliwa kiajali, wanaweza kusababisha madhara kwa afya ya binadamu kwani wana minyoo hatari.

Kulingana na ripoti kutoka kwa afisa msimamizi wa Mradi wa Mpunga Mwea, Bw Innocent Ariemba, wadau katika Kaunti ya Embu wamekuwa wakitafuta mbinu kukabiliana na konokono hawa ili kuzuia uharibifu zaidi.

Hadi sasa, wamevamia ekari 1,000 kati ya 26,000 katika eneo hilo. Hula mipunga kwa pupa kama kwamba wamo vitani. Aidha, wanazaana kwa haraka sana na huwahangaisha wakulima pakubwa. Hili bila shaka ni janga kuu linalokodolea Kenya macho.

Kwamba kuna wakulima wengine ambao walilazimika kupanda mimea yao tena baada konokono hawa kutafuna mipunga waliyopanda katika awamu ya kwanza ni thibitisho la hasara ambayo wakulima wameanza kupata kutokana na mdudu huyu mharibifu.

Jopo lililoundwa kukabiliana na konokono hawa limependekeza mbinu mbalimbali kama vile utumiaji wa kemikali, kuwaondoa moja kwa moja ama kutumia wadudu wanaowala ili kuwaangamiza kabisa. Tayari kuna hofu mavuno msimu ujao yatakuwa ya chini ikilinganishwa na kipindi sawa mwaka jana. Asilimia kubwa ya mchele nchini hutoka eneo hili na iwapo serikali haitachukulia tatizo hili kama janga jipya, huenda nchi ikakumbwa na baa la njaa miaka michache ijayo.

Iwapo hatua za haraka zingechukuliwa Februari, wakati konokono hawa walivamia Mwea, wangekuwa wameangamizwa.

Bw Awino ni mtaalamu wa mawasiliano na mhariri msanifishaji wa zamani katika Taifa Leo