Makala

AWINO: Mageuzi kuhusu mbolea yafaa, lakini mambo bado

March 10th, 2020 2 min read

Na AG AWINO

TANGAZO la Waziri wa Kilimo Peter Munya kwamba amevunjilia mbali kundi la wafanyibiashara ambao wamekuwa wakiagiza mbolea kwa niaba ya serikali katika mradi wa utoaji wa mbolea kwa bei nafuu ni hatua mwafaka katika kuboresha sekta ya kilimo nchini.

Chini ya mradi huu, wakulima wamekuwa wakiuziwa mbolea kwa Sh3,200 badala ya Sh2,300 ambayo ndiyo bei ambayo wakulima sasa watakuwa wakinunua chini ya mpango mpya kutoka kwa serikali.

Mwaka jana, kulingana na Bw Munya, Kenya ilipoteza Sh2 bilioni kwenye mradi huo wa mbolea.

Huenda Waziri amepanga kupiga chenga vikundi ambavyo vimekuwa vikicheza karata katika mpango wa utoaji wa mbolea kwa bei nafuu na kuleta hasara kwa mkulima na hii ni hatua ya kupigiwa kongole.

Hata hivyo, licha ya waziri kujikakamua kuimarisha mfumo wa utoaji wa mbolea, kumekuwa na tetesi pia kuhusu viwango vya ubora wa mbolea inayotolewa na serikali na pia wingi wa kemikali zenye sumu. Pia sharti aangazie suala hili anapolainisha utoaji wa mbolea.

Kuna baadhi ya wakulima ambao walisusia matumizi ya mbolea ya serikali baada ya kugundua haifaia mazao yao, na badala yake wakajinunulia mbolea kwa bei za juu kutoka maduka ya kibinafsi.

Pengine hoja ambayo haijawekwa wazi kwa wakulima kuhusu mbolea ya serikali ni kwamba licha ya kuwa zina kiwango cha chini cha ubora, huwa na virutubishi vingine muhimu ambavyo hufaidi zaidi mazao yanayovunwa baada ya mwaka mmoja na zaidi kama vile miwa, majani chai, kahawa na pareto.

Mimea inayokomaa chini ya mwaka mmoja kama mahindi, maharagwe, mboga na nyanya ndiyo haisaidiwi na mbolea hii.

Matokeo ya matumizi ya mbolea inayonunuliwa kwenye maduka ya kibinafsi na zile za serikali huwa wazi haswa zinapotumika kwenye mashamba jirani yenye mimea sawa. Utapata mimea ya shamba moja imenawiri huku mimea ya shamba jirani imesinyaa.

Waziri sharti atilie mkazo miradi ya kuleta mbolea inayofaa mimea mbalimbali katika maeneo tofauti nchini. Haifai kuwapa wakulima mbolea ambayo haiwezi kufaidi mazao yao.

Wakati umewadia wa kuleta mabadiliko ya kudumu katika kilimo kama vile kuleta pamoja wawekezaji ili kujenga viwanda vipya vitakavyotengeza mbolea iinayohitajika kwa mazao mbalimbali katika kila sehemu nchini.

Hatua za haraka za kisiasa hazitaleta mabadiliko ya kudumu katika kilimo nchini kwani kupunguzwa kwa bei ya ununuzi wa mbolea ni asilimia kidogo tu ya mikakati inayohitajika kuimarisha kilimo na hali ya mkulima kwa jumla.

[email protected]