Makala

AWINO: Serikali itekeleze ahadi yake kwa viwanda vya miwa

September 24th, 2020 2 min read

Na AG AWINO

KABLA Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya atangaze kwamba, serikali ilikuwa inatafuta wawekezaji wa muda wa kampuni tano za sukari zinazomilikiwa na serikali, alichapisha kanuni mpya kusimamia sekta hii.

Kwenye mwongozo huo, miwa ilijumuishwa rasmi pamoja na mimea kama mpunga, majani chai, pareto na kahawa.

Siku chache baadaye, alitangazwamba serikali ilikuwa imefutilia mbali madeni kampuni hizo zilikuwa zimelimbikiza kama hatua mojawapo ya kuwavutia wawekezaji. Madeni hayo ni pamoja na ushuru ambao Halmashauri ya Ushuru Nchini (KRA) ilikuwa ikidai.

Baadaye, Halmashauri ya Chakula na Kilimo (AFA) ilitangaza kutafuta wawekezaji kupiga jeki kampuni hizo.

Hata hivyo, kabla wawekezaji 15 ambao walipita awamu ya kwanza ya mchujo kutajwa rasmi, Chama cha Wafanyikazi Katika Sekta ya Miwa (KUSPAW), kilitangaza kuenda mahakamani kupinga hatua hii ya serikali hadi mwakilishi wao ateuliwe kwenye kamati ya urasimu ya wakurugenzi wakuu watano wa kampuni za Nzoia, SoNy, Chemelil, Muhoroni na Miwani pamoja na wawakilishi wa Wizara ya Kilimo.

Mojawapo ya masharti ilikuwa chama hicho cha wafanyakazi kiondoe kesi zote kortini.

Hali hii ilitia hofu wadau wengine kama vile katibu wa Umoja wa Wakujazi Miwa Nchini (KSGA) Bw Paul Ogendo ambaye aliomba Kuspaw iondoe kesi mahakamani ili shughuli ya kutafuta mwekezaji iendelee.

Chama cha Wakuzaji Miwa Nchini (NASFO) nacho pia kilihimiza KUSPAW kuondoa kesi hiyo kortini. Kauli ya wakuu hawa ni kwamba, wawekezaji wapya wataleta mabadiliko katika biashara ya miwa na kuwakomboa mikononi mwa kampuni za kibinafsi ambazo zimekuwa zikiwafyonza wakulima kutokana na ukosefu wa ushindani.

Wiki jana, ilibainika kwamba licha ya KUSPAW kuahidi kuondoa kesi yao mahakamani, bado hawajafanya hivyo wakisema wanasubiri serikali kutimiza pia masharti mengine.

Ikumbukwe kwamba, kwamba katibu mkuu wao sasa ni mwanachama wa kamati ya urasimu baada ya jina lake kuchapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali.

KUSPAW haifai kuondoa kesi hii mahakamani hadi serikali itimize masharti yao. Wiki mbili zilizopita KRA ilifunga akaunti za Nzoia na Chemelil licha ya madeni yao kufutiliwa na Bw Munya.

Hatua kama hizi ni ishara onyo tosha kwamba, njia bora zaidi kujikinga na mijeledi ya serikali ni kupitia mikataba na mkondo wa kisheria namna KUSPAW inafanya.

Iwapo Serikali haitatimiza masharti ya Kuspaw huenda wafanyikazi wakapoteza haki zao kwa kiwango kikubwa wawekezaji wapya watakapochukua usukani.