Makala

AWINO: Ushuru unaotozwa bidhaa za kutoka nje uwe kwa zote

November 5th, 2020 2 min read

Na AG AWINO

KILA mwaka Kenya huagiza mahindi, sukari, ngano, mchele na vyakula vingine kwa kushindwa kuzalisha cha kutosheleza wananchi wake.

Ingawa serikali imekuwa ikiweka mikakati ya kuzuia kuingizwa kwa vyakula visivyo bora, mianya bado ipo mpakani Busia, Namanga na Malaba.

Kwa mfano, ingawa serikali ilifunga mwanya wa kuingiza sukari ya nje kama mojawapo ya njia za kupiga jeki soko la wakulima wa humu nchini, kuna sukari nyingi tu inapita kimagendo.

Habari kwamba sasa ni hatia kuagiza ngano kutoka nje kabla zao la nchini kutumika, ni njema sana kwa wakulima.

Aidha, wasagaji ngano sharti wasubiri hadi ngano ya nchini iishe kabla kuagiza ya kutoka nje, la sivyo, wataadhibiwa. Lakini wakifuata masharti haya, watalipa asilimia kumi tu ya ushuru wa bidhaa, ikilinganishwa na wanaoagiza mapema ambao hutozwa asilimia 35 zaidi ili kuzima tamaa ya wasagaji kukimbilia masoko ya nje ili wafaidike haraka wakipuuza mazao ya wakulima wa humu nchini.

Ingawa kuna tetesi kwamba wapo wafanyabiashara wanaoenda kinyume na matakwa haya, jambo linaloshangaza ni sheria tofauti kwa bidhaa za kilimo nchini.

Ni kweli kila mmea una changamoto zake na wahitaji kanuni zake binafsi; lakini suala kama la ushuru linafaa kuwa sawa kwa wakulima wote bila kubagua.

Imekuwa wimbo kwamba kilimo kinakabiliwa na matatizo chungu nzima hasa kutokana na ushuru unaotozwa katika viwango mbalimbali vya uzalishaji na uuzaji mazao.

Ingawa adhabu ya ushuru ni hatua nzuri, haiwezi kuzuia wasagaji kuagiza ngano kutoka nje kwani ushuru wa juu, unaotokana na ushuru unaotozwa katika kila kiwango cha uzalishaji, ni gharama ambayo msagaji husukumia wanunuzi. Kwa hili, ni dhahiri kwamba mlio wa chura haujamzuia ng’ombe kunywa maji.

Ingawa lengo la vikwazo vya ushuru ni kuwakinga wakulima dhidi ya bei duni, tusisahau kwamba kiburi ni mali ya mwenye uwezo na hiari.

Wadau wote wa kilimo na hasa Kamati ya Kilimo katika Baraza la Magavana (CoG) ikiongozwa na Gavana wa Tharaka Nithi Muthomi Njuki, inafaa kupendekeza sheria ambazo hazitaonekana kupendelea sehemu moja ya wakulima.

Chapati au maandazi hayaliwi pekee mezani, lazima kuambatana na kitoweo cha maharagwe, pojo, nyama na kinywaji cha kuteremsha kama vile chai.

Hivi vyote ni vyakula ambavyo visipolindwa vyema kiushuru, hatimaye anayeumia ni mkulima mkuzaji na mwananchi mnunuzi.

Yafaa sheria iwekwe kwa mazao yote nchini. Inashangaza kwamba hata majani chai, kahawa na mazao mengine yanayozalishwa kwa wingi humu nchini sasa yanaagizwa kutoka nje kwa sababu ushuru wa kuingiza ni nafuu kuliko unaotozwa kila hatua ya uzalishaji.

Wabunge hawana budi kupitisha sheria ya ushuru wa juu kabisa kwa kila bidhaa inayoagizwa kutoka nje ambayo inakuszwa humu nchini, ili watu wazoee kutumia mazao na vifaa vya humu nchini.

La sivyo, wafutulie ushuru huu kwa bidhaa zote.

AG Awino ni mwanamawasiliano anayeandika kuhusu masuala ya kilimo

[email protected]