Makala

AWINO: Viwanda vya Sukari: Wanaodai maoni tena huenda hawana nia njema

October 8th, 2020 2 min read

Na GILBERT AWINO

KABLA serikali kuhitimisha mpango wake we kutafuta wawekezaji katika sekta ya sukari, wapo watu ambao tayari wameanza kuishinikiza kuhusisha wananchi katika mpangilio huu wa kutafuta wawekezaji katika sekta ya miwa.

Ilibidi Katibu katika Wizara ya Kilimo Bi Anne Nyagah kuahidi kwamba shughuli ya kukusanya maoni ya wananchi kulingana na kipengele cha kumi cha Katiba itafanywa.

Yapo manufaa mengi ambayo yanaletwa na ukusanyaji wa maoni katika mradi wowote wa serikali kwani huchangia katika kuwapa maarifa wananchi kuhusu madhumuni ya serikali.

Tatizo lililopo hata hivyo ni kwamba, kabla serikali kuamua ni hatua gani, inaonekana wapo wale ambao wanadai kwamba kukusanya maoni yao tena ila tu kwa wakati huu, nia yao ni kukwamiza shughuli za kutafuta wawekezaji.

Uamuzi wa kutafuta wawekezaji wa muda katika sekta ya miwa uliafikiwa baada ya mapendekezo ya Tume ya Ubinafsishaji kugonga mwamba. Ilibidi rais abuni kamati ambayo ilikusanya maoni ya wananchi kuhusu namna ya kufufua sekta ya miwa nchini. Wakati wa kukusanya maoni, tume ambayo kwa wakati huo ulikuwa unaongozwa na hayati Henry Obwocha ilijipata katika hali ngumu kwani kila walipotafuta maoni ya wananchi, walizomewa na watoa maoni ambao hawakutaka kusikia chochote kuhusu ubinafsishaji wa kampuni hizi.

Baadaye tume iliyoongozwa na Oparanya ilipoanza kukusanya upya maoni kuhusu matatizo ya miwa, pia walitembea kila eneo ili kusikia maoni ya wananchi. Walipomaliza, Rais aliangalia pia mapendekezo yao na kuamua kwamba ni vyema kutafuta tu mwekezaji wa muda badala ya kuuza kampuni hizi moja kwa moja.

Kwa hivyo, wanaodai kwamba maoni ya wananchi haikukusanywa ni wasiosema ukweli. Hata hivyo, katiba haisemi ni mara ngapi wananchi wanafaa kuhusishwa kwa hivyo hakuna kinachomzuia Wizara ya kilimo kutembea na kukusanya maoni ya wananchi tena.

Kwamba serikali imekuwa ikikubali na kusikia matakwa ya wadau mbalimbali katika shughuli hii ya kutafuta mwekezaji ni jambo la kupigiwa upatu.

Tunafaa hata hivyo kujihadhari na watu ambao lengo lao ni kutumia ukusanyaji wa maoni kama njia mojawapo ya kukwamiza jitihada za kufufua sekta hii. Watu wasiokuwa na habari yoyote kuhusu uendeshaji wa viwanda ndio mara nyingi hupinga na kukataa kusikia ujumbe kuhusu uwekezaji kwa sababu wanatumiwa na watu wenye nia mbaya

Miaka michache iliyopita,Tume ilizuru eneo la magharibi kukusanya maoni ya wakulima kuhusu uwekezaji. Usiku wa kuamkia shughuli hiyo, wadau wengine walipanga na kupiga msasa orodha ya watu ambao wangepewa nafasi ya kutoa maoni yao. Mmoja baada ya mwengine aliambiwa kwamba wasikulali ubinafsishaji.

Wakati ulipofika, Bw Obwocha na wenzake walibaki vinywa wazi kwani msemaji baada ya mwengine alikataa mapendekezo yao na hata kuambiwa apeleke mapendekezo ya uwekezaji huko Kisii alikozaliwa. Licha ya kwamba aliendelea kuzungumza, tayari alikuwa ameonyeshwa madharau. Ukweli ni kwamba mara nyingi wachache wanaofaidika kutokana na hali mbaya ya kampuni hizi hutafuta kila njia kuhakikisha ya kwamba hatua yaoyote inayopendekezwa ya ufufuzi haifiki mwisho.

Kuweka kampuni za serikali mikononi mwa wawekezaji kutaongeza ushindani miongoni mwa viwanda vingine vilioko majirani na mashirika haya yanayoogopa ushindani. Watafanya kila njia kuchelewesha ushindani. Aidha, siasa ya mwaka wa 2020 sasa imeanza kushuhudiwa katika maeneo ya miwa kwani kuna wengine ambao wanaona ni vizuri shughuli za kutafuta wawekezaji unafaa kuahirishwa hadi baada ya uchaguzi wa 2022.

Ni aibu kwamba Nchi ya Uganda hutengeneza sukari kiasi cha kutosha ambacho kinauzwa humu nchini. Nchini Tanzania, viwanda vyote vinavyofanya vizuri ni vya kibinafsi. Iwapo serikali na wadau wenye nia njema hawatasimama imara wanaotaka sana maoni yao yakusanywe ni wanafiki ambao watajaribu kila njia kukwamiza mabadiliko katika sekata ya sukari.

Bw Awino ni mwanamawasiliano anayeandika kuhusu kilimo

[email protected]