Makala

AWINO: Wakuzaji miwa waige wenzao wa mahindi

July 23rd, 2019 2 min read

Na GILBERT AWINO

Ripoti kutoka Bodi ya Sukari nchini yaonyesha kwamba katika kipindi cha miezi sita iliyopita, serikali iliagiza sukari takribani tani 200 elfu.

Katika kipindi sawa na hiki mwaka jana, serikali iliagiza tani 99 elfu. Ongezeko hili ni asilimia 102.

Sukari inapoangizwa, bei ya sukari nchini inapungua na kuchangia mkulima kutopata faida ya kilimo chake cha miwa.

Kwa mfano, kutokana na sukari hii iliyoagizwa, bei ya gunia moja ya Sukari ilipungua kutoka kwa Sh4,600 hadi Sh4,300.

Matatizo mengi

Matatizo ambayo wakulima wa miwa hukumbana nayo ni mengi sana. Hata wanapolipwa kwa wakati, mapato yao huwa kidogo na yasiyoweza kubadilisha maisha yao. Wanaishi maisha ya uchochole na taabu nyingi sana.

Mkulima wa miwa kila mara akiwa na shida, huwa ‘analilia serikali’ kufanya hivi ama vile.

Si ajabu kuwaona wakulima wa miwa wakipiga foleni nyumbani kwa wanasiasa ili matatizo yao yatatuliwe na wao hao wanasiasa ambao huwa wanaagiza sukari kutoka nje na kuzidi kuchangia kudorora maisha yao. Ni sawa na kondoo kutafuta haki mbele ya fisi!

Wanaamini kwamba wakililia wanasiasa, matatizo yao yatakwisha. Uwongo mkubwa! Haiwezekani.

Wakulima wa mahindi

Kumekuwa na tetesi kwamba wakulima wa mahindi nchini hudekezwa na kusikilizwa zaidi kuliko wakulima wa kahawa, miwa na mazao mengine.

Hivi majuzi, Waziri wa Kilimo Bw Mwangi Kiunjuri alikuwa katika vyombo vya habari kutokana na ripoti kwamba alikuwa amefanya mipango ya kuagiza mahindi ya bei nafuu kutoka Mexico. Habari ilipotokea, wakulima wa mahindi hawakulilia serikali, walipiga vita juhudi hizi.

Kwanza kupitia mwenyekiti wa Hifadhi ya Chakula Nchini ,Bw Noah Wekesa walipiga kelele na kupinga vikali mpango huu. Bw Wekesa hakuogopa kwenda kinyume na mkubwa wake. Akasimama kidete na kusema kwamba kuna mahindi ya kutosha nchini.

Pili kupitia Bungeni, walishawishi wanachama wa Kamati ya Kilimo na Mifugo bungeni kuagiza Bw Kiunjuri kusitisha mara moja mipango yoyote ya kuagiza mahindi kwa sababu kuna mahindi ya kutosha nchini.

Mwaka jana, Wabunge wa Seneti walikuwa na wakati mgumu sana wakiwa Eldoret walipokutana ana kwa ana na wakulima wa mahindi. Kwa jazba na ghadhabu, wakulima walitoa onyo kali kwa wabunge hao na kuwaonya dhidi ya kupuuza mkulima wa mahindi. Waliwashinikiza kuzingatia changamoto zao bila kulalamika. Hawakuwalilia Wabunge hawa kwa onyonge na machozi. Pengine walielewa kwamba mnyonge hana haki.

Ni wazi kwamba wakulima wa mahindi wanaelewa mbinu ya kuvutia kwao. Serikali imeonyesha kwamba inawasikiliza tu waliowajibika na kudai haki yao bila kuogopa.

Umoja

Umoja ambao umeshuhudiwa miongoni mwa wakulima wa mahindi ni tofauti sana wenzao wa miwa ambao kila mara hawazungumzi kwa sauti moja.

Huku wengine wakitetea, kwa mfano, kurejeshwa kwa maeneo, wengine hawataki.

Tumewaona wakiuana na kuibiana miwa wenyewe kwa wenyewe. Hawana siri kati yao. Kila vikundi vyao huenda kwa Waziri wa Kilimo na viongozi mbalimbali wakiwa na hoja zinazokinzana.

Kushusha Bei

Sawa na sukari, mahindi kutoka Mexico huwa ni bei ya chini na kila yanapoingia humu nchini hushusha bei ya gunia la mahindi na hivyo kusababisha mkulima kutoweza kupata faida ya uwekezaji wake katika kilimo cha mahindi.

Wakulima wa miwa wamekuwa wakilalama kwamba sukari inapotoka nje, wao ndio huumia zaidi. Uagizaji mwingi umeathiri wakulima wa miwa na hata ni hatari kwa wananchi kwa sababu wakati fulani si salama kwa afya ya wananchi.

Wakulima wa miwa sharti waige wenzao wa mahindi ambao wamegundua kwamba mbinu mwafaka katika kulinda sekta ya mahindi ni kusimama kidete na kupiga nduru wakidai haki bila ‘kuomba serikali’. Enzi za kulilia serikali kwa msaada ulikwisha kwani kila mwamba ngoma sharti avutie kwake.

Bw Awino ni mtaalamu wa mawawasiliano katika sekta ya kilimo nchini