Makala

AWINO: Wanaoshiriki kilimo bila ujuzi wasaidiwe kwa ushauri

August 13th, 2020 2 min read

Na AG AWINO

SASA ni dhahiri kuwa shule hazitafunguliwa mwaka huu 2020 na matumaini yamewekwa kwa mwaka 2021 ikiwa ugonjwa wa Covid-19 utakuwa umedhibitiwa.

Hii ina maana kuwa zaidi ya walimu na wahadhiri 400 wataendelea kukaa nyumbani hadi mwaka 2021. Zaidi ya nusu ya idadi hii wanaishi mashambani.

Kuna idadi kubwa ya walimu hawa ambao huwa hawafanyi kazi yoyote mbadala kama njia mojawapo ya kujiinua zaidi kiuchumi. Lakini kufuatia kufungwa kwa shule kwa kipindi kirefu sasa wako na nafasi ya kufanya mengine yenye manufaa kifedha.

Pia takwimu zaonyesha kwamba zaidi ya watu milioni moja wamepoteza kazi zao kutokana na athari za corona. Asilimia kubwa ya watu hawa wamehamia mashambani baada ya maisha kuwa magumu mijini.

Hata hivyo, kuna manufaa ambayo yameandamana na janga la corona. Kwa mfano, watu waliokuwa wamesahau jamii zao mashambani sasa wamejumuika nao, na mashamba ambayo hayakuwa yakilimwa sasa yanalimwa na hivyo kuongeza kiwango cha chakula kinachokuzwa nchini.

Pia baadhi ya watu ambao hawakuwa na ari yoyote katika kilimo wameingilia ukulima na ufugaji kama njia mojawapo ya kuongeza mapato au kwa kukosa lingine la kufanya. Hawa wote ni wakulima limbukeni.

Lakini ulimbukeni huu katika kilimo usipoongozwa ipasasvyo unaweza ukachangia madhara zaidi badala ya faida kwani hawana ujuzi wa shughuli hii muhimu.

Kwa mfano kuna suala la matumizi ya kemikali za kilimo ambazo ni hatari kwa afya ya binadamu na mazingira. Kumekuwa na tetesi kwamba baadhi ya vyakula vinavyopewa vifaranga ili kukua kwa haraka vimechanganywa na dawa za kupunguza makali ya Ukimwi.

Pia baadhi ya kemikali zinazotumika shambani kuzuia magugu na kuua wadudu zimethibishwa kusababisha matatizo mengi kiafya ikiwemo ugonjwa wa saratani. Hii ndiyo sababu mashirika kama Food to Action yameanza kutetea matumizi ya mbolea ya wanyama.

Kinachohitajika zaidi kwa sasa, ni kwa serikali kuimarisha mafunzo kuhusu mbinu za kilimo zinazofaa kwa wakulima hawa limbukeni.

Maarifa kuhusu vyakula vinavyofaa kwa mifugo pia sharti yaongezwe kupitia vyombo vya habari na maafisa wa nyanjani. Hii itasaidia kuhakikisha chakula kinachozalishwa ni salama na mavuno yanaongezeka.

[email protected]