Michezo

Ayub Masika Timbe sasa ni mali ya Reading FC

February 1st, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

NI rasmi winga klabu ya Beijing Renhe nchini China, Ayub Masika Timbe, sasa ni mali ya Reading FC inayoshiriki Ligi ya Daraja ya Pili nchini Uingereza.

Timbe, 27, alijiunga na Reading katika siku ya mwisho ya kipindi kifupi cha uhamisho hapo Januari 31 kwa mkopo wa miezi minne. Kandarasi hiyo itamweka uwanjani Madejski hadi mwezi Mei 31, 2020.

Reading inamilikiwa na bwanyenye Dai Yongge kutoka nchini Uchina. Yongge pia ndiye mmiliki wa Beijing Renhe.

Timbe amekuwa Renhe tangu Februari 20, 2017, alipojiunga na klabu hiyo kutoka Lierse nchini Ubelgiji ambako alikuwa ameishi kutoka mwaka 2010 na pia kuchezea klabu za Beerschot na Genk pamoja na kupata uraia wa nchi hiyo.

Mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Kenya ya Harambee Stars alikuwa Reading kwa majuma kadha akifanyiwa majaribio na kuvutia kocha Mark Bowen.

“Masika ni mchezaji aliye na talanta ya hali ya juu na kasi ya kutisha ambayo inaweza kudhuru wapinzani,” Bowen alimsifu.

Timbe alikuwa kwenye rada ya Reading tangu mwaka 2019, lakini mpango wa kujiunga nayo mwaka huo ulitatizwa na masuala kadha katika kandarasi yake. Hata hivyo, masuala hayo yanaonekana yametatuliwa, huku habari nchini Uingereza zikidai kuwa anafanyiwa uchunguzi wa kiafya kabla ya kusaini kandarasi ya miezi mitano.

Winga huyo wa pembeni kulia hakuwa na msimu mzuri 2019 baada aliposumbuliwa na majeraha na pia kushuhudia Beijing Renhe ikitemwa kutoka Ligi Kuu. Tovuti ya Transfermarkt inaweka thamani ya Timbe sokoni wakati huu kuwa Sh72 milioni.

Reading imekuwa katika Ligi ya Daraja ya Pili kwa misimu saba.

Inashikilia nafasi ya 15 kwa alama 37 kutokana na mechi 29 kwenye ligi hiyo ya klabu 24. Timbe hajakuwa sawa kutokana na kuwa ligi ya China imekuwa likizoni.

Hata hivyo, huenda akahusishwa katika mechi ijayo ya Reading ambayo ni dhidi ya Cardiff City katika raundi ya nne ya Kombe la FA mnamo Februari 4.