Azidi kumiminiwa sifa kwa kutumia talanta yake katika michoro kusaidia nyanya kupata haki

Azidi kumiminiwa sifa kwa kutumia talanta yake katika michoro kusaidia nyanya kupata haki

Na SAMMY WAWERU

MCHORAJI mmoja nchini ameendelea kumimiwa sifa chungu nzima kwa kutumia kipaji chake katika uchoraji kusaidia nyanya kupata haki ya fidia baada ya kuondolewa katika shamba lake ili kuruhusu mradi wa maendeleo kutekelezwa.

Bw Joseph Maina alichora picha ya ajuza Jane Nyambura ambaye video yake akilalamikia kuhujumiwa na kampuni moja ya Kichina katika kijiji cha Kariua, Gatundu Kaskazini, Kaunti ya Kiambu, ilisambaa mitandaoni Januari 2021.

Akimlaumu mmoja wa wafanyakazi katika kampuni hiyo iliyopewa zabuni kuchimba Bwawa la Karimenu, Bi Nyambura alisema aliondolewa bila kupewa fidia kikamilifu.

“Nilifukuzwa hapa na China…nilipoondolewa niliahidiwa fidia ila sikuipata…” akasema kupitia video iliyoenea.

“Jambo ambalo nitasema, nionyewe yule msichana…yule nionyewe kwa sababu ninaweza kufanya tendo la ajabu..” Nyanya Nyambura Wa Kiragu akaelezea kwa hasira, akinyooshea kidole cha lawama mfanyakazi aliyedai kuchangia mahangaiko yake.

Video hiyo ilionekana kuzua ucheshi, ila ajuza huyo alikuwa analilia haki yake.

Mchoro wa Joseph Maina ulisaidia nyanya Jane Nyambura Wa Kiragu kupata haki baada ya kuondolewa kwenye shamba lake ili kuruhusu ujenzi wa Bwawa la Karimenu, Gatundu Kaskazini, Kaunti ya Kiambu. Picha/ Sammy Waweru

Bw Joseph alitumia talanta yake akachora picha ya Nyambura, lugha ya mchoro ikionyesha nyanya mwenye hamaki.

“Baada ya kuipakia katika kurasa zangu za mitandao, ilienea kama moto unavyochoma nyasi nyikani. Watu wakaanza kunipigia simu wakitaka kujua kilichojiri, wengine wakinipa oda niwachore,” akaambia Taifa Leo wakati wa mahojiano katika karakana yake Ruiru, Kiambu.

Alisema ni kupitia mchoro huo Bi Nyambura ameahidiwa na serikali kupata fidia.

“Nilipomtembelea na kumtunuku picha hiyo, alinisimulia alivyohangaika kupata haki, hata hivyo, hatimaye alinifichulia atapata fidia baada ya nyumba yake kubomolewa na shamba lake kutwaliwa na serikali kuruhusu mradi wa Bwawa la Karimenu kutekelezwa,” Joseph akasema.

Ujenzi wa Karimenu unatarajiwa kugharimu kima cha Sh24 bilioni.

Ni kupitia jukwaa la msanii huyo kusaidia nyanya Nyambura kupata haki Joseph ameendelea kupongezwa na wananchi.

“Mungu akujaalie kwa kutia nyanya tabasamu apate haki,”@Winfred Mwirigi akamhongera.

“Michoro ina hadithi, pongezi kwa kazi nzuri,” akaelezea Patrick Rotich, naye Peter Mwaura Kabiku akiridhia talanta ya barobaro huyo kusaidia Bi Nyambura kupata haki.

You can share this post!

Fowadi Moise Kean awabeba PSG hadi ndani ya 32-bora French...

Boateng kukosa fainali ya Kombe la Dunia kati ya Bayern...