Habari Mseto

Azimio langu ni kufikia upeo wa Mercy Johnson, asema Dorcas Gatuna

February 11th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

”SIKU moja mtaiona sura yangu kwenye runinga.’ Haya ni matamshi yake Dorcas Mwihaki Gatuna akifunguka alivyozoea kuwaambia wazazi wake akiwa mdogo.

Hata hivyo, nao walikuwa wakimuunga mkono kwani alikuwa akionyesha dalili za kuibukia uigizaji jambo lililoendelea kumtia moyo zaidi.

Anajivunia kutimiza ndoto hiyo ambapo ameshiriki muvi kibao ambazo zimefanikiwa kurushwa kupitia runinga tofauti hapa nchini ikiwamo Kameme TV na Inooro TV.

”Muvi yangu ya kwanza ilipeperushwa kupitia Inooro TV mwaka 2014 iliyofahamika ‘Msichana tajiri’ nilioshiriki chini ya Discovery Media Productions,” alisema na kuongeza kwamba hatua hiyo ilimfanya kujawa furaha tele.

Gatuna ameshiriki muvi zaidi ya 20 chini ya brandi kadhaa ikiwamo Pama Productions, Prima Pictures na Discovery Media Productions.

Katika mpango mzima Gatuna anasema ana matumaini ya kufanya kazi za nguvu ndani ya miaka mitatu na unusu ijayo. Anasema amepania kuionoa talanta yake akilenga kutinga levo ya kimataifa ili kupata mialiko kufanya kazi na mastaa tofauti katika mataifa ya kigeni kama Tanzania, Nigeria na Afrika Kusini kati ya nchi zinginezo.

”Mimi nimejiwekea azimio moja kuu: kujitahidi na kutinga levo ya staa mahiri ambaye huigiza muvi za Kinigeria (Nollywood) Mercy Johnson maana hufanya kazi zake bila kupigia chini nafasi yoyote ya ushiriki wake.

Licha ya kushiriki nafasi yoyote ambayo hutwikwa katika uhusika wake nyakati zote huonyesha heshima ya ubinadamu kama kawaida kando na uigizaji,” alisema.

Kwa kuhofia kubomoa ndoa yake anasema nyakati zote anapotarajia kushiriki muvi inayogusa masuala ya mahusiano ya kimapenzi mwanzo wa ngoma utangulia kumfahamisha bwanake.

”Mimi nina familia changa ambapo kabla sijashiriki muvi sampuli hiyo lazima nimjulishe bwanangu kusudi azizue rabsha pengine akishuku kumfanyia mchepuko,” alisema.

Baadhi ya muvi ambazo ameshiriki ni: Mwana ti kironda (Mtoto sio kidonda), Rugano rwa Karendi (Hadithi ya Karendi) na Iceera ria Mami (ziara ya mama yangu) kati ya zinginezo.

Mwigizaji huyu anaishukuru serikali kwa kuhidhinisha taifa hili kuwa na mfumo wa mashirika mengi ya habari kinyume na iliyokuwa miaka iliyopita. Mfumo huo umechangia wananchi wengi kupata ajira tofati katika vyombo vya habari nchini.

”Kiukweli mfumo huo umechangia kuwepo ushindani mkubwa hali inayonitia motisha zaidi maana inalenga kupaisha tasnia ya muvi na filamu,” alisema na kuongeza kwamba waigizaji wa Kenya wanapiga hatua wanakolenga kufikia wenzio wa muvi za Hollywood.

Mwigizaji huyu anaitaka serikali kupunguza kodi ambayo hutozwa brandi za husika wanapolenga kushuti muvi zao mijini. Anashauri wazazi wawe mstari wa mbele kuwaunga wanao mkono badala ya kuwavunja moyo wanapotambua talanta zao.