Azimio wampa Ruto msururu wa matakwa

Azimio wampa Ruto msururu wa matakwa

NA JUSTUS OCHIENG’

KIONGOZI wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga, jana Jumatano aliwaongoza viongozi wa muungano huo na wafuasi kutoa matakwa makali kwa serikali ya Rais William Ruto akitisha kuwa raia watachukua hatua kali yasipotimizwa.

Katika mkutano wa kwanza wa kujadiliana na wafuasi wake katika uwanja wa kihistoria wa Kamukunji jijini Nairobi, Bw Odinga alionya kuwa “Wakenya watakuwa huru kuchukua hatua watakazotaka kupunguza mzigo wa minyororo waliyotwikwa mabegani mwao” na utawala wa Kenya Kwanza.

Kwenye maazimio yaliyosomwa na Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Bw Opiyo Wandayi, Viongozi wa Azimio wanataka serikalli ichukue hatua za kupunguza gharama ya bidhaa muhimu hasa kwa kurudisha ruzuku ya unga, mafuta na stima wakisema mojawapo ya ahadi za kampeni za Rais Ruto ilikuwa ni kupunguza bei ya unga na gharama ya maisha.

“Kwa sasa tunayoshuhudia ni kinyume, bei ya unga haijashuka na walichofanya ni kuondoa ruzuku za mafuta na kufanya Wakenya kubeba mzigo zaidi wa gharama ya maisha,” alisema Bw Odinga.

Katika mkutano uliohudhuriwa na vigogo wa muungano huo wa upinzani wakiwemo Kalonzo Musyoka, Martha Karua, Eugene Wamalwa na Wycliffe Oparanya, viongozi hao waliitaka serikali kudumisha ruzuku ya karo ya shule za sekondari kuanzia mwaka ujao.

“Ruto anafaa kufahamu kwamba, huenda mambo yamekuwa bora kwa watu wachache, lakini sio kwa maelfu ya wazazi, ukweli wa mambo ni kuwa hali ya uchumi imekuwa mbaya,” akasema Bw Odinga.

Ili kupatia raia wa mapato ya chini afueni ya mzigo wa gharama ya maisha, viongozi wa Azimio wanataka serikali ya Kenya Kwanza kurudisha mpango wa Kazi Mtaani ambao ulianzishwa na serikali ya Jubilee kukinga vijana dhidi ya athari za janga la corona.

Mwezi Novemba, Rais Ruto alifuta mpango huo akisema vijana watakuwa wakifanya kazi katika mpango wa ujenzi wa nyumba nafuu na “sio kuokota takataka”.

Kazi Mtaani, ilihusisha vijana kudumisha usafi wa mazingira katika miji mikubwa kote nchini.

Aidha, Bw Odinga aliitaka serikali ya Kenya Kwanza kurudisha pesa za kinga ya wazee chini ya mpango wa Inua Jamii na Mpango wa Afya ya Uzazi wa Linda Mama ambao ulisaidia akina mama kujifungua hospitalini bila kutozwa ada.

Wazee waliosajiliwa chini ya mpango wa Inua Jamii walikuwa wakipata Sh2000 kila mwezi kutoka kwa serikali.

Azimio wanataka serikali ya Rais Ruto kukomesha mara moja kuwazia uagizaji wa mahindi yaliyobadilishwa maumbile kisayansi maarufu (GMO) na kukoma kutangaza masuala muhimu ya sera kiholela.

Kulingana na Bw Odinga hatua hii inatokana na ukosefu wa uwazi katika sera za serikali.

“Wakenya watakuwa huru kukataa kutii maagizo na masuala yanayotolewa kiholela na maafisa wa serikali,” akasema.

Wakidai kuwa serikali ya Kenya Kwanza inateka nyara taasisi huru, vigogo wa Azimio waliitaka serikali kuheshimu na kukumbatia utawala wa sheria hasa katika mchakato wa kuunda Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

“Ikikosa kufanya hivi, Wakenya watakuwa huru kuchukua hatua zitakazowazesha kuafikia lengo hili,” alisema Bw Odinga.

Matakwa mengine ya Azimio kwa serikali ni kukoma kuondoa kesi za washukiwa wa uhalifu, kukoma kulazimisha vijana kuchukua mikopo ya Hazina ya Hasla na kuhakikisha watumishi wa umma wanawakilisha sura ya taifa badala ya kuteuliwa kwa upendeleo na ukabila.

  • Tags

You can share this post!

Mbunge amshambulia Winnie Odinga

Kaunti zalilia mabilioni ya uchumi wa baharini

T L