Azimio wasisitiza kuwa mapambano yataendelea

Azimio wasisitiza kuwa mapambano yataendelea

NA WINNIE ONYANDO

VIONGOZI wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya wamesema kuwa wataendelea kupambana hadi watakapopata haki.

Wakiongozwa na kinara wa ODM, Raila Odinga, viongozi hao walisema kuwa tayari wamekubaliana kuhusu hatua ya kuchukua ya kupinga matokeo ya urais yaliyotangazwa Jumatatu.

“Tumejadiliana kama muungano na tumekubaliana kutumia mbinu ya kisheria kuwasilisha malalamishi yetu kuhusiana na matokeo yaliyotangazwa na mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC), Wafula Chebukati,” akasema Bw Odinga.

Kwa upande wake, kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka aliwataka Wakenya kutopoteza matumaini kwani safari ya kupata haki imeanza.

Alisisitiza kuwa wataendelea kupambana hadi muungano wao utakapopata haki.

“Hatujapoteza matumaini. Tuna imani kuwa haki itatawala katika suala hilo. Tunawaomba Wakenya waendelee kusimama nasi hadi tamati,” akasema Bw Musyoka.

Kadhalika, aliwaomba Wakenya kuendelea kudumisha amani hata wanapojiandaa kuwasilisha malamalishi yao kortini.

“Tuwe kitu kimoja. Tuungane mikono ili pamoja tupate haki,” akasema Bw Musyoka.

Naye mgombea mwenza wa Bw Odinga, Martha Karua aliwahakikishia Wakenya kuwa watapata ushindi.

Alisema kuwa japo Bw Chekubati alimtangaza Naibu wa Rais, Willima Ruto kuwa Rais mteule, na kuwapokonya ushindi, muungano wa Azimio utapata ushindi.

“Muungano wa Azimio una idadi kubwa ya wabunge katika serikali ya juu. Hii inaonyesha kuwa tunatawala. Nawahakikishia Wakenya kuwa tutapata ushindi,” akasema Bi Karua.

Haya yanajiri siku chache baada ya Bw Odinga kupinga matokeo yaliyotangazwa na Bw Chebukati akidai siyo ya kikatiba.

  • Tags

You can share this post!

Aliyetumia wilbaro kama jukwaa ni MCA

Ruto ikulu katika jaribio la kwanza

T L