Habari za Kitaifa

Azimio yadai serikali ilifadhili ghasia zilizotokea wakati wa maandamano


MUUNGANO wa Azimio One Kenya umemtaka Rais William Ruto kutia saini Mswada wa Sheria wa Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi (IEBC) 2024 ili kuandaa nchi kwa uchaguzi kutokana na maandamano ya hivi majuzi dhidi ya serikali nchini.

Vinara wa muungano huo wakiongozwa na kiongozi wa chama cha Wiper Democratic Movement Kalonzo Musyoka wanasema Rais William Ruto anafaa kuitisha uchaguzi wa haraka.

“Wakenya tayari wameeleza kutokuwa na imani na serikali hii na tunamtaka Rais Ruto aidhinishe mswada huo kuwa sheria ili kuwaruhusu Wakenya kutekeleza haki zao za kidemokrasia kwa kuwafanya viongozi kuwajibika. Wabunge wanaogopa hata kwenda bungeni kutokana na matukio yanayoshuhudiwa huko. Atie sahihi mswada huo ili Wakenya waondoe wabunge na kupisha uchaguzi wa haraka,” Bw Musyoka alisema.

Kuhusiana na maandamano ya hivi majuzi nchini, Bw Musyoka alilaumu serikali kwa ‘kufadhili wahuni’ ambao walijipenyeza katika maandamano ya amani na kusababisha uharibifu wa mali na mauaji.

“Haya yalikuwa maandamano ya amani ya Gen Z dhidi ya serikali lakini tumeona kuwa kuna vurugu ‘zinazofadhiliwa na serikali’ na kukodisha wahuni kwa nia ya kuharibu sifa ya maandamano,” akaongeza.

Muungano huo pia umedai kuwa ghasia hizo zinazofadhiliwa na serikali zinanuiwa kumfanya Rais Ruto atangaze hali ya hatari na kusimamisha Katiba.

Maandamano ya hivi majuzi yaliyoongozwa na Gen Z yalilenga kuzima Mswada wa Fedha wa mwaka 2024 ambao ulipingwa na watu wengi na pia kulalamikia ufisadi na kutaka utawala bora nchini.

Rais William Ruto aliitikia shinikizo wiki jana na kuuondoa Mswada wa Fedha wa 2024. Dkt Ruto pia amesema yuko tayari kufanya mazungumzo na vijana hao ili kutatua baadhi ya masuala ambayo bado hayajakamilika ambayo wameibua kuhusiana na uongozi wa nchi.

Maandamano hayo kufikia sasa yamesababisha vifo vya waandamanaji 39 na kujeruhi wakenya zaidi ya 300 kote nchini.

Katika taarifa aliyotoa kivyake, kiongozi wa ODM Raila Odinga aliitaka serikali kuanza uchunguzi mara moja kuhusu uharibifu wa mali na matukio ya wizi yaliyoshuhudiwa wakati wa maandamano ya Jumanne.

Waziri mkuu huyo wa zamani alishutumu utawala wa Rais William Ruto kwa kusita kuwachukulia hatua washukiwa waliosababisha ghasia Jumanne.

Odinga alisema kuwa serikali ilikuwa na taarifa za kutosha kuhusu wafadhili wa maandamano yanayoendelea lakini imechagua kutowachukulia hatua.

Kulingana naye, maandamano yaliyoshuhudiwa Jumanne ambayo yalihusisha uharibifu na wizi yalikuwa tofauti na yale yaliyoshuhudiwa mwanzoni mwa maandamano ya Gen Z.

“Kwa majambazi kuteka nyara maandamano na kuyageuza kuwa ghasia dhidi ya Wakenya wasio na hatia ni sawa na usaliti maradufu wa vijana. Tabia hii mbaya inapaswa kukomeshwa,” Raila alisema.

“Watu ambao sio Gen Z walioanzisha maandamano waliyateka, wakapora biashara, wakashambulia Wakenya wasio na hatia na kuharibu miundombinu muhimu,” aliongeza