Habari za Kitaifa

Azimio yalaumu serikali kwa kuchelewesha fedha za kupiga jeki elimu

March 20th, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

KUNDI la wabunge wa muungano wa Azimio la Umoja–One Kenya limeitaka serikali kutoa pesa ambazo shule za upili zinaidai.

Wabunge hao walisema mnamo Jumanne kwamba kuchelewesha kwa pesa hizo kunahujumu masomo katika taasisi hizo.

Wakiongozwa na Kiongozi wa Wachache katika Bunge la kitaifa Opiyo Wandayi, wabunge hao watapatao 10 walimsuta Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu kuwa kutotoa tarehe kamili ambapo pesa hizo zitatumwa shuleni.

Mnamo Jumatatu, Katibu katika Wizara ya Elimu Belio Kipsang’ aliiambia Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Uhasibu (PAC), kwamba serikali itatuma Sh16.25 bilioni kwa shule za upili ndani ya siku 10 zijazo.

Kiasi hicho kinawakilisha asilimia 25 ya Sh32.5 bilioni za mpango wa elimu bila malipo kwa shule za upili ambazo serikali ilistahili kutuma katika shule hizo muhula huu wa kwanza ulipoanza Januari 8, 2024.

“Tuko hapa kuikaripia serikali kwa uongo wake ambao umelemaza shule za upili na kuwaacha walimu wakuu na wazazi wakilaumiwa na wazazi na wanafunzi wanaoamini uongo wa serikali,” Bw Wandayi akawaambia wanahabari katika majengo ya bunge.

Mbunge huyo wa Ugunja alifichua kuwa shule za msingi na za upili zinadai serikali jumla ya Sh52.8 bilioni ambazo ni malimbikizo ya tangu 2021.

“Ni makosa zaidi kwa serikali kuvuruga masomo ya wanafunzi kwa kunyima shule ufadhili. Ni wajibu wa kikatiba wa serikali kufadhili elimu ya msingi ya watoto wote nchini,” akasema Bw Wandayi.

Mbunge huyo wa chama cha ODM alihusisha matokeo mabaya ambayo yamekuwa yakiandikishwa katika Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) miaka minne iliyopita ya ufadhili finyu wa shule za upili nchini.

“Hali katika shule zetu ni mbaya zaidi. Matokeo ya haya yote ni kwamba viwango vya elimu vitashuka nchini, hali ambayo itaathiri mustakabali wa watoto wetu,” akaeleza huku akibashiri kuwa huenda mgomo ukatokea katika shule za upili nchini kutokana na changamoto za kifedha zinazoathiri taasisi hizo.

Mbunge wa Kitui ya Kati Makali Mulu alisikitika kuwa serikali kuu inaelekeza kiasi kikubwa cha pesa kwa mipango na miradi isiyo ya dharura na kutelekeza sekta ya elimu.

“Mbona sekta nyingine zinazosimamiwa na serikali kuu zinapata pesa zao kwa wakati ilhali pesa za sekta ya elimu zinacheleweshwa? Hii ina maana kuwa serikali hii haithamini masomo ya watoto wetu ilhali hawa ndio nguvukazi itakayotegemewa kusukuma gurudumu la maendeleo nchini,” akasema.

Kwa upande wake, mbunge wa Nyando Jared Okello aliitaka serikali kuongeza mgao wa fedha za mpango wa elimu bila malipo katika shule za msingi na upili wakisema mgao wa sasa ni ndogo mno.

“Mgao wa sasa wa Sh1,245 kwa kila mwanafunzi katika shule za upili na Sh22,224 katika shule za upili uliwekwa mnamo 2017. Kiwango hiki cha pesa ni ndogo zaidi ikizingatiwa kuwa gharama ya maisha imepanda,” akaeleza.

Lakini huku wabunge wa Azimio wakiibua malalamishi hayo, Dkt Kipsang Jumatatu aliwaambia wanachama wa PAC kwamba serikali imelazimika kupunguza mgao wa fedha kwa kila mwanafunzi katika shule za upili kutoka Sh22,224 kila mwaka hadi Sh17,500.

“Hii imetokana na ongezeko la idadi ya wanafunzi katika shule za upili kwa kiwango cha 1 milioni. Mgao wa Sh65.25 bilioni ambao serikali imetenga mwaka huu hautatosha jumla ya wanafunzi 4.2 milioni walioko katika shule za upili ikiwa ni lazima wao kutengewa Sh22,224. Hii imetulazimisha kupunguza mgao kwa kila mwanafunzi hadi Sh17,500,” Dkt Kipsang akasema.

Katibu huyo alifichua kufikia Januari 2024, idadi ya wanafunzi katika shule za upili iliongezeka kutoka 3.2 milioni hadi 4.2 milioni.