Azma ya Kalonzo itamfaidi mgombea mwingine, asema Kibwana

Azma ya Kalonzo itamfaidi mgombea mwingine, asema Kibwana

Na CHARLES WASONGA

GAVANA wa Makueni Profesa Kivutha Kibwana amepuuzilia mbali tangazo la kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kwamba atawania urais akisema hatua hiyo itamfaidi Naibu Rais William Ruto.

Kwenye taarifa aliyotuma kwa vyombo vya habari Jumapili, Januari 16, 2022, Profesa Kibwana alisema hatua hiyo pia itamnyima Raila Odinga kura za eneo la Ukambani.

“Mkakati wake ukifaulu, William Ruto ndiye atafaidi. Kwa kujua au kutojua, Kalonzo atakuwa amemsaidia mgombeaji ambaye huenda akafanya kazi naye baadaye,” akasema Prof Kibwana.

Profesa Kibwana alisema haikuwa na haja kwa Bw Musyoka kutangaza atakuwa debeni kuwania urais kwani atapata kura za eneo la Ukambani pekee wala sio pembe zote za nchini.

“Katika uchaguzi mkuu wa 2007 ikiwa Kalonzo hangewania urais kungekuwa na mshindi wa moja kwa moja kati ya Rais mstaafu Mwai Kibaki na kiongozi wa ODM Raila Odinga. Hii “KUPITA KATIKATI” ndio ilichangia matokeo ya uchaguzi wa urais mwaka huo kuzua ubishi,” akasema.

Gavana huyo alisema hayo siku moja baada ya Bw Musyoka kuongoza mkutano mkubwa wa viongozi kutoka Ukambani nyumbani kwake, Yatta, Machakos.

Ni katika mkutano huo, ambapo alitangaza kuwa atawania urais huku akielezea matumaini ya kupata uungwaji mkono kutoka kwa vinara wenzake wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA).

Kiongozi huyo wa Wiper alipata uungwaji mkono kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kidini kutoka eneo hilo.

Hata hivyo, Profesa Kibwana alisema viongozi wa Ukambani Christian Leaders Forum na wanachama wa Baraza la Wazee hawakuwakilishwa katika mkutano huo na hivyo “hauna uhalali.”

“Nia ya Kalonzo ni kutumia jina la jamii ya Wakamba na sehemu za kura 1.6 milioni za eneo hili kuchuuza kwa wangombeaji wakuu wa urais, kwa manufaa yake binafsi. Hii ni kwa sababu anafahamu fika kwamba hana uungwaji mkono maeneo mengine ya nchi,” gavana huyo akaeleza.

  • Tags

You can share this post!

AFCON: Sierra Leone walazimishia Ivory Coast sare ya 2-2...

WANDERI KAMAU: Siasa zimeidunisha na kuteka taaluma ya...

T L