Dondoo

Azomea mama kutaka aite wapenziwe ‘uncle’

March 5th, 2018 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

NGARA, NAIROBI

Kioja kilizuka kwenye ploti moja mtaani humu, kijana alipomzomea mama yake kwa kumlazimisha kuwaita makalameni aliokuwa akitembea nao ‘uncle’.

Kulingana na mdokezi, kijana hakupendezwa na tabia aliyokuwa akionyesha mama yake. Duru zinasema mara kwa mara mama ya kijana alikuwa akifika nyumbani usiku akiandamana na mwanaume.

Penyenye zinasema mama alikuwa akimwambia mwanawe kuwa kila mwanamume aliyeandamana naye alikuwa ‘uncle’ yake.

Inadaiwa kwamba, siku ya tukio mama kijana aliingia kutoka safari zake za kawaida akiandamana na jamaa fulani. “Huyu ni uncle wako. Ataenda kesho,” mama alimweleza mwanawe.

Kijana alibaki ameduwaa. “Mum tangu lini huyu akawa mjomba wangu. Huyu jamaa mimi namfahamu vizuri sana,” kijana alimueleza mama yake kwa hasira.

Inasemekana mama alianza kumzomea mwanawe huku akimuonya dhidi ya kumchunga.

“Mimi sikuchungi. Huyu jamaa ni mlevi mashuhuri anayejulikana na kila mtu hapa,” kijana alimuambia mamake.

Kulingana na mdokezi, kijana alimueleza mamake amuonyeshe babake aliyemzaa. “Mambo ya kulazimishwa kuwaita watu uncle hapa sitaki. Nionyeshe babangu,” kijana aliteta.

Mama alibaki mdomo wazi. “Kila wakati unakuja hapa na watu mbalimbali. Unaniambia niwaite uncle. Kwani hawa uncle kwenu ni wangapi?” kijana alimkaripia mamake.

Inadaiwa mama alimuonya mwanawe akome kumdhalilisha la sivyo angemtimua. Kijana naye hakutishwa na maneno ya mama yake.

“Wewe umezidi sasa. Huyu unayetaka nimuite uncle akiondoka kesho, lazima unionyeshe ninayestahili kumuita baba na pia nataka kujua wajomba wangu wote,” kijana alimueleza mamake. Inasemekana kijana aliondoka na haikujulikana ikiwa mama alikoma kuwaalika wanaume alivyokuwa amezoea.