Michezo

Azpilicueta lawamani Kepa kukaidi Sarri kwa fainali

February 25th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

BAADHI ya Mashabiki wa Chelsea wamemfokea vikali naibu nahodha wa timu hiyo Cesar Azpilicueta kuhusiana na kisa tata kilichomhusisha kocha Maurizio Sarri na mnyakaji Kepa Arizzabalaga katika fainali ya Kombe la Carabao dhidi ya Manchester City usiku wa Jumapili Februari 24.

Arrizabalaga alikataa kuondoka uwanjani dakika za mwisho mwisho katika muda wa ziada ya fainali hiyo ugani Wembley ili kupisha nyani mwenzake Willy Caballero ambaye alitazamiwa kuingia ili kunyaka penalti za wapinzani.

Tukio hilo limepelekea idadi kubwa ya mashabiki kumvamia Azpilicueta wakisema alifaa kutumia uongozi wake uwanjani kumtoa kipa huyo kwa lazima ili Caballero ambaye ni mnyakaji mahiri wa mikwaju ya penalti awaokoe na kuwapa ubingwa wa taji hilo.

Azpilicueta ambaye ni naibu wa Garry Cahill aliyelishwa benchi kutokana na kiwango chake cha chini ya mchezo, alikera mashabiki aliposema hakuona vizuri tukio hilo na hawezi kutoa uamuzi kulihusu.

“Kwa uaminifu, mimi sikushuhudia vizuri kilichotokea. Nilikuwa upande mwingine wa uwanja na siwezi kuzungumzia tukio lenyewe,” akasema Azpilicueta.

Hata hivyo ,shabiki kwa jina Jake Kimberly akasema “ Bado vitendo vya Kepa vimeniudhi. Nasikitikia kocha kutokana na lawama ambazo amekuwa akimiminiwa ilhali ni wachezaji kama hawa ndio hukosa kumtii. Ingekuwa Terry ndio yupo uwanjani kama nahodha basi kipa huyo angetoka hata kwa kubururwa. Azpilicueta hafai kusalia na utepe wa unahodha kwa sababu alikosa kudhihirisha mamlaka yake,”

Manchester City hata hivyo walishinda mechi hiyo kwa mabao 4-2 na kubeba kombe hilo kwa mwaka wa pili mfululizo.