Dondoo

Azua rabsha kipusa alipodinda kumnengulia kiuno

October 11th, 2018 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

Baba Ndogo, Nairobi

K IZAAZAA kilizuka katika baa moja mtaani hapa baada ya polo kuomba wahudumu wamtimue kipusa aliyekataa kujumuika naye jukwaani kunengua mauno.

Minong’ono yasema polo alikasirishwa na mrembo kukataa kucheza naye baada ya kuteremsha chupa kadhaa za pombe aliyomnunulia.

Kulingana na mdokezi, polo aliingia katika baa na kuanza kujivinjari. Mrembo naye aliwasili na kuketi kwa meza nyingine iliyokuwa karibu na jamaa na kuitisha maji.

“Sasa mrembo, njoo uketi hapa,” polo alimrai mrembo. Mrembo naye bila kupoteza wakati, alimsongea jamaa.

“Unakaa mrembo sana. Haufai kunywa maji. Itisha kinywaji unachotaka,” jamaa alimueleza kipusa. Polo alimuita mhudumu na kuitisha pombe.

Duru zinasema mambo yalianza kuharibika pindi tu muziki ulipoanza kuchezwa. Inadaiwa polo aliinuka na kuanza kubanjuka. Mwanadada alikuwa ameketi tu huku akiendelea kuteremsha kinywaji.

Inasemekana jombi alimshika mrembo mikono akitaka ainuke ili wacheze naye lakini mrembo hakuinuka. “Kwani hutaki kucheza na mimi?” polo alimuuliza mrembo.

Kipusa hakumjibu polo naye akaamua kuketi chini na kuziondoa zile chupa za pombe zilizokuwa mbele ya mrembo.

“Huwezi kuendelea kula mali yangu na hutaki kuongea nami. Pia umekataa kusakata ngoma na mimi,” jamaa alimfokea mrembo.

Mrembo aliinuka na kuanza kumzomea polo. “Ni wewe uliniita hapa na ukaninunulia pombe. Sikuitisha. Cheza peke yako,” mrembo alimkaripia polo.

Penyenye zinasema polo alizusha akitisha kumuangushia mrembo makofi. Baa iliyokuwa tulivu ilibadilika ghafla jamaa akiwataka wahudumu kumfurusha mwanadada huyo.

“Huyu demu ni mjinga sana. Amekunywa pombe yangu chupa saba na anakataa kucheza na mimi. Mfukuzeni hapa kabla sijamuangamiza,” polo aliwaeleza wahudumu wa baa ambao walimwambia alifaa kufukuzwa mwenyewe kwa kuzua vurugu.