Makala

Baa kuu la njaa lazua utapiamlo na kuumiza wakazi Pokot Magharibi

April 3rd, 2018 5 min read

Na OSCAR KAKAI

MAJERAHA kwenye vichwa na nyuso za watoto sita yanakukaribisha unapoingia katika boma la Josephine Chepang’ole Kakuko ambaye anajulikana kwa wengi kama Mama Kibet.

Watoto wenye utapia mlo wako katika hali mbaya na wanahitaji msaada wa chakula, wanahitaji msaada wa dharura.

Watoto hao na mama yao ambaye ni tegemeo la pekee na karibu ajifungue wakati wowote, ndiye anashughulikia wanawe sita, wa saba karibu azaliwe.

Ndani kwenye nyumba watoto wawili wamekaa sakafuni katika kijiji cha Kaizagat eneo la Paraiywa wadi ya Siyoi kaunti ya Pokot Magharibi.

Watoto wengine wanne wanapiga miayo, wamedhoofika, wachafu, wamekonda, wanaonekana wagonjwa wakikaa kwenye jua nje ya nyumba yao wakitiririkwa na machozi.

Familia hiyo ya maskwota, haina malazi wala nguo, vyombo havina chakula chochote.

Watoto hao wenye umri kati ya miaka miwili na saba wanaonekana kana kwamba hawajala kwa kipindi cha mwezi mzima.

Kifungua mimba aliacha shule akiwa darasa la nne, wa pili aliachia darasa la pili, wa tatu na wa nne ambao ni mapacha hawajawahi kuenda shuleni.

Mama huyo anabeba kitinda mimba anayeonekana mwenye huzuni na mawazo tele na haonyeshi dalili yakutaka kutukaribisha.

Jirani yao Bw Nicodemus Siwatum ambaye ni mwandishi kwenye mitandao, anasema kuwa familia hiyo iliachwa baada ya baba yao Bw Francis Obae Ekidor kufungwa kwa miaka miwili.

“Siku ya kwanza nilipokuja hapa, macho ya watoto hawa yalikuwa meupe pe pe pe na hawakuwa na uwezo wa kutembea sababu miguu yao ilikuwa imefura.

Nilishikwa na huruma na nikalazimika kuweka taarifa hiyo kwa mtandao wa Facebook kuhusu hali yao,” alisema Bw Siwatum.

Alisema kuwa wasamaria wema wamekuwa wakifika katika boma hilo kusaidia familia hiyo na chakula. Nyumba hiyo ambayo wanaishi ndani walipewa na msamaria mwema

Mbunge wa Kapenguria Bw Samuel Moroto ambaye aliguswa alichukua mtoto mmoja kwa jina Mercy Chebet na kumpeleka shuleni.

“Niliguswa na yale ambayo niliona kwenye mtandao vile watoto hawa walikuwa wanaumia,” alisema.

 

Hawajala wiki nzima
Jirani mwingine Bw Kibet Parklea anasema kuwa watoto hao hawajakula kwa wiki nzima sasa.

“Nilitiririkwa na machozi wakati nilifika katika boma hili siku ya kwanza. Tuliwapa chakula na nguo lakini bado wanahitaji msaada,” alisema Bw Kibet.

Akiongea na Taifa Leo, afisa wa lishe bora katika kaunti, Bi Jane Limang’ura, anasema kuwa utafiti wa hivi majuzi kuhusu utapia mlo katika kaunti hiyo uliofanywa na shirika la Unicef, Action For Hunger (ACF) na Wizara ya Afya unaonyesha kuwa kiwango cha utapia mlo katika kaunti hiyo ni asimilia 39.9 ambao ulifanywa Juni 2017.

Bi Limangura anasema kuwa kiwango hicho kimerudi chini baada ya kuwa juu kutokana na lishe mbaya katika kaunti hiyo.

“Kuna mbinu mbaya za lishe na akina mama wa kaunti hii,” akasema. Hospitali ya kaunti ya Kapenguria hupokea kati ya watoto 70 -100 kila mwezi wa utapia mlo.

 

Watoto wafupi

Karibu watoto nusu chini ya miaka mitano katika kaunti hiyo ni wafupi wa kimo, na thuluthi yao wako na kilo za chini kwa uzito kulingana na utafiti wa hivi majuzi wa Kenya Demographic and Health Survey.

Kiwango cha kitaifa cha utapia mlo ni asilimia 26 na uzito wa asilimia 11.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa elimu katika kaunti, Bw Jarred Oberio alisema kuwa kuna chakula cha kutosha kwenye shule za eneo hilo na hakuna haja ya malalamishi.

“Shule zote katika kaunti ndogo ya Pokot ya kati zinapewa chakula na shirika la kusambaza chakula duniani la World Food Program. Kuna mchele, unga wa uji na mahidi. Tulisambaza chakula katika maeneo ya Kong’elai, Sook, Chepareria maeneo mengine ya Pokot ya ya kati. Pengine kuna njaa nyumbani na wala sio shuleni ” alisema.

Tume ya kupambana na ufisadi nchini [EACC] ilisimamisha kuondolewa kwa mahindi magunia elfu mia tano ambayo yalinunuliwa na serikali ya kaunti hiyo ambayo yamezuiliwa katika bodi ya kuhifadhi mazao na nafaka ya Kacheliba kwa madai ya kutofuata utaratibu kwenye ununuzi wa mahindi hayo yalinunuliwa nje ya kaunti hiyo mwanzoni mwa mwaka huu.

Mahindi hayo yalistahili kugawiwa wahanga wa njaa, huku wakazi wakilaumu viongozi wa eneo hilo kwa kuingiza siasa kwenye suala hilo.

Wakazi hao wanaitaka serikali kuingilia kati na kutatua sakata hiyo ya mahindi ambayo imezuiliwa katika ghala la kuhifadhi mahindi, ili yatolewe yaweze kugawa kwa wanaoathiriwa na njaa.

 

Wakulima wanaumia

Wakazi hao walisema kuwa wanaumia kutokana na uhaba wa chakula baada ya kukosa kuvuna mazao kipindi cha upanzi kilichopita kutokana na mvua ndogo iliyonyesha katika eneo hilo na sasa wanataka suala hilo kutatuliwa.

“Tulikuwa na furaha tulipoona mahindi yakinunuliwa na sasa tunashangaa mbona hatupewi. Hatupandi mahindi sababu mvua kidogo hunyesha eneo hili,” alisema Bw Lorita.

Alishangaa ni kwa nini mahindi hayo hayajapeanwa kwa wakazi wanaokabiliwa na baa la njaa huku wakikabiliwa na uhaba wa chakula.

“Mbona tusipewe mahindi ? Tunauliza serikali shida ni nini ilihali tunaumia na njaa? Tunaambukizwa na magonjwa na mayatima wanaumia. Wale ambao wanapiga kelele wameshiba,” alisema.

Akiongea katika eneo la Turkwel, Gavana Prof John Lonyangapuo alizisuta taasisi za serikali kwa kutotatua mzozo huo wa mahindi huku wakazi wakiumia na njaa.

Alisema kuwa serikali ya kaunti hiyo hajalipia mahindi hayo baada ya tume ya kupampana na ufisadi (EACC), DPP na polisi kuingilia suala na kusimamisha mchakato huo.

Gavana Lonyangapuo alisema kuwa serikali ya kaunti hiyo ilitenga fedha za kununua mahindi hayo na kuwaweka kwenye maghala ili yatumiwe wakati wa njaa.

“Mbona wakora wanasema kuwa ununuzi wa mahindi haukuwa na uwazi ilhali watu wetu wanakufa na njaa? Tunapeana mahindi kidogo ilihali kuna mahindi ya kutosha kwenye ghala. Watu hapa wanakaa wiki nzima bila kula,” akasema.

Prof Lonyangapuo aliitaka serikali kuu kuingilia suala hilo na kusadia wakazi na chakula msaaada.

 

‘Wakora’

Gavana huyo alisema kuwa wale wanashtumu serikali ya kaunti hiyo kwa ununuzi wa mahindi hayo ni wakora ambao walikuwa wakiiba kwenye serikali iliyopita.

“Walikuwa wakinunua mahindi kwa Sh8,000 kwa kila gunia ilihali sisi tulinunua kwa Sh4,000. Wale ambao wanapinga ununuzi wa mahindi ni wapinzani wetu ambao walifeli kwenye uchaguzi ulipoita na hawataki maendeleo eneo hili,” akasema.

Alisema kuwa wakazi wa eneo hilo wanakabiliwa na uhaba wa chakula sababu hawakuvuna kwenye msimu wa upanzi uliopita baada ya mazao yao kuharibu na wadudu

Chifu wa Ombolion, Bw Joseph Korikimul alitaka msaada wa kibinadamu ili kuokoa wakazi wa eneo hilo.

“Shule nyingi katika eneo hili zinakabiliwa na njaa. Wanafunzi wanalazimika kuondoka shuleni. Mayatima na wajane ndio wanaumia zaidi,” akasema.

Waziri wa kilimo na mifugo katika kaunti hiyo, Bw Geoffrey Lipale anasema kuwa wamefanya utafiti katika kaunti nzima na asilimia themanini ya kaunti hiyo inakabiliwa na uhaba wa chakula.

“Maeneo ambayo yameathika zaidi ni Riwo, Kacheliba katika kaunti ndogo ya Pokot Kaskazini, Masol, Turkwel na nyanda za chini za Sook katika kaunti ndogo ya Pokot ya kati. Shirika wa chakula Duniani (WFP) na Unicef walifanya uchunguzi na kutoa ripoti kama sawa kama yetu,” alisema.

Bw Lipale alitoa wito kwa mashirika ya kijamii kusadia kusambaza chakula cha msaada katika maeneo ambayo yameathirika.

 

Hali inazorota

“Wakazi wengi wanakabiliwa na makali ya njaa na hali hii inaendelea kuwa mbaya kila uchao. Hawana chochote cha kukula na wanategemea chakula cha msaada kutoka kwa serikali na mashirika ya kijamii kujikimu. Tunaomba serikali ya kaunti kuingilia kati na kuokoa hali hiyo. Hatuwezi kungoja hadi watu wafe.

Mwezi mbaya huwa wa sita lakini mambo yameanza mapema na hali huenda ikawa mbaya zaidi,” akasema.

Waziri huyo alitoa wito kwa serikali kuu kupitia kwa idara ya kushughulikia kiangazi, majanga na mashirika mengine kuingilia kati kufanya uchunguzi na kuweka mikakati ya kutatua shida hiyo.

Mbunge wa Kacheliba Bw Mark Lomunokol alisema anashangaa kuona mashamba na mazao kunyauka sababu ya ukosefu wa mvua.

“Wakazi wa Kacheliba sasa wako katika hatari ya njaa kwa miezi ijayo,” akasema.

Alitoa wito wa msaada wa chakula kwenye shule za eneo hilo, ili kuzuia wanafunzi kuacha shule.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Sarimach, Bw Wilson Lonoki anaitaka serikali kusambaza chakula katika shule za eneo hilo.

Bw Lonoki alitilia shaka suala la wanafunzi kukosa chakula kwenye shule akisema kuwa wengi wamelazimika kuondoka shuleni.

Alisema kuwa shule zinakosa chakula kuwaweka wanafunzi shuleni.

 

Bila chakula hawaendi shuleni

“Watoto katika maeneo ya mpaka huenda shuleni wakati kuna chakula. Bila chakula wao huamua kukaa nyumbani. Hii imechagia kudorora kwa viwango vya elimu licha amani kupatikana eneo hili. Shule zimeathirika na masomo huenda yakalemazwa ikiwa hali hii itaendelea hivi,” alisema Bw Lonoki.

Joshua Lokienyang, mkazi wa Kacheliba anasema walipanda mbegu mbaya, jambo analoamini ndilo lililochangia kuwepo kwa mavuno duni.

“Mvua kidogo ilinyesha na mazao hayakufanya vyema,” alisema Lokienyang.

Kaunti ya Pokot Magharibi ina idadi ya wakazi 800,000 wanaoishi katika eneo kame, ambapo mvua kidogo hunyesha kila mwaka.

Kulingana na halmashauri ya kupambana na kiangazi nchini [NMDA] na wizara ya kilimo katika kaunti hiyo kati ya wakazi 70,000 na 250,000 wa kaunti wanakabiliwa na baa la njaa baada ya mazao yao kufeli kutokana na kiangazi ambacho kilishuhudiwa katika eneo hilo na udongo duni.

Maeneo ambayo yameathirika zaidi ni kaunti ndogo za Pokot Kaskazini na Pokot ya Kati.

Takwimu kutoka kwa idara ya kilimo katika kaunti hiyo zinaonyesha kuwa zaidi ya wakazi 140,000 wanakabiliwa na uhaba wa chakula.