Makala

BAA LA NJAA: Watumiaji mitandao ya kijamii waelekeza huko kero zao

March 19th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

KAUNTI 13 ndizo zimeripotiwa kuathirika zaidi na baa la njaa linalotokana na ukame unaoendelea kushuhudiwa nchini Kenya.

Serikali Jumatatu ilitangaza kwamba imetenga Sh2 bilioni ili kuangazia ama kwa maneno mengine kukabiliana na hali ya makali ya njaa katika kaunti hizo zinazohitaji msaada wa dharura.

Naibu Rais Dkt William Ruto akitoa tangazo hilo katika afisi yake jijini Nairobi alikiri kuwa watu 1,111,500 wamekabiliwa na hali ngumu ya ukosefu wa chakula na maji.

Serikali imekanusha taarifa kuwa zaidi ya watu tisa kufikia sasa wamefariki kwa sababu ya njaa.

Inasema maafa ya waliofariki yametokana na magonjwa ila si njaa.

Dkt Ruto alisema hakuna haja ya kuzua taharuki, akihoji kwamba taifa lina chakula cha kutosha.

“Hakuna haja ya kuzua hofu, hali si mbaya kama ilivyokuwa miaka miwili iliyopita,” akasema Dkt Ruto.

Alisema serikali kuu inashirikiana na serikali za kaunti kuratibu bajeti ili kuhakikisha kila Mkenya anapata chakula na maji.

Janga la njaa si jambo geni nchini. Hali inayoshuhudiwa sasa si ya kwanza na ya pili, wala ya tatu.

Umekuwa wimbo “tumetenga fedha kukabili ukame” kila makali ya njaa yanapotangazwa. Ni kinaya kauli hiyo ikiradidiwa baadhi ya wananchi wakifa njaa.

Idara ya utabiri wa hali ya anga kwa upande wake inahoji ilikuwa imetoa tahadhari kwa serikali uwezekano wa kuwepo kwa mafuriko na ukame.

Kuna kitengo cha kukabiliana na majanga nchini, NDMU, na ambacho kwa kiasi fulani kinaonekana kuzembea hasa kutokana na hali inavyoonekana.

Watumiaji na wafuatiliaji habari na matukio katika mitandao ya kijamii wameelezea kero za, wakishangaa wenzao kufa njaa ilhali viongozi wao wanaonekana kujitia hamnazo.

Waathiriwa pia walishiriki shughuli ya kidemokrasia kuchagua viongozi.

Kinachowauma zaidi ni kuona wenzao wakifa ilhali mabilioni ya pesa yanaendelea kufujwa.

“Uhalifu wa fedha za umma umekuwa ratiba ya kila siku Kenya, huku wenzetu wakiendelea kuangamizwa na ukame. Mungu anaona wote wanaofuja pesa zetu, wenzetu wakifa,” Mercy Mbaabu amelalamika kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Katika siku za hivi karibuni, visa vya ufisadi vimeripotiwa kukita mizizi, Wakenya wakizitaka asasi husika kunusuru mali ya umma kukaza kamba ili yarudishwe kusaidia wananchi.

“Hii ni aibu iliyoje mataifa ya kigeni yakiona Wakenya wakihangaishwa na njaa (huku) pesa za umma zikifujwa?” anauliza Emmy Keira.

Wakulima kutoka kaunti tajika za ukuzaji wa nafaka nchini wanasema wana mahindi mengi ambayo serikali ikikubali kuyanunua yote, yataokoa wahanga wa njaa.

Turkana

Baringo, Pokoto, Turkana, na Marsabit ni baadhi ya kaunti zilizoathirika pakubwa.

Gavana wa Pokot Magharibi Profesa John Lonyangapuo na ambaye pia ni mkulima anasema serikali itafutie wakulima wa mahindi soko, akidokeza kwamba wamekosa mahala pa kuyapeleka. Hii ni licha ya bodi ya kitaifa ya nafaka, NCPB, kuyanunua ingawa kwa kipimo.

“Serikali kuu haijaweka mikakati bora kuangazia matakwa ya wakulima, hasa soko la mazao. Ikusanye pesa, inunue mahindi yote kisha iyapeleke kwa waathiriwa wa njaa,” anahimiza Profesa Lonyangapuo.

Kulingana na gavana huyu ni kwamba wakulima eneo la North Rift wana mahindi mengi kiasi cha kukosa maghala ya kutosha kuyahifadhi.

Kiongozi huyu hata hivyo, anahimiza Wakenya kuendelea kujitolea kusaidia walioathirika kwa vyakula.

“Nimetoa magunia 700 ya mahindi yaelekezwe maeneo ya Tiaty Baringo, Pokot ya Kati na Kaskazini, ambayo ukame umekithiri. Ninaomba wananchi tushirikiane kuokoa wenzetu,” ashauri.

Ili kuangazia suala la njaa siku za usoni, Profesa Lonyangapuo anapendekeza serikali za kaunti kupiga jeki wakulima kwa kuwapa mbegu na mbolea bila malipo.

Awali, Pokot Magharibi ilikuwa miongoni mwa kaunti zilizokumbwa na baa la njaa na anasema alipochukua usukani 2017, kila mwaka hutoa mbegu bila malipo kwa zaidi ya wakulima 200,000.

Ni hatua ambayo imeonekana kubadilisha taswira ya kaunti hiyo.