Makala

Baa zee katika eneo la Pwani

October 6th, 2020 3 min read

Na DIANA MUTHEU

TANGU Jumatatu wiki jana baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kuwa wamiliki wa baa, vilabu na maeneo mengine ya burudani wanaweza kurejelea biashara zao miezi sita baada ya kufungwa kama mojawapo ya mikakati iliyotolewa kuzuia maambukizi ya virusi vya corona, sehemu nyingi tayari zimeanza kazi na wateja wanamiminika kukata kiu ya pombe.

Hata hivyo, baadhi ya maeneo hayo bado hayajafunguliwa kwa sababu kama vile; wanasubiri idara ya afya ya umma ije ikague maeneo hayo, wengine wanaendelea kutafuta vifaa vya kuwasaidia kupambana na maradhi ya Covid-19 kama vile sabuni, maji, na vipima joto.

Mojawapo ya baa ambazo hazijafunguliwa ni Kilindini iliyoka kando ya barabara ya Mwakilingo, Mombasa ambayo ndiyo baa zee kabisa katika eneo la Pwani, na nchini kwa jumla.

Mwaka huu 2020 baa hiyo inajivunia miaka 112 ya kutoa huduma kwa watu mbalimbali.

Baa hiyo imekuweko mojawa ya vivutio vya watalii katika Kaunti ya Mombasa kwa kuwa ina historia ndefu.

Kwa sasa, inamilikiwa na Maura De Souza Abranches, ambaye alirithi biashara hiyo mnamo mwaka wa 2016 baada dadake, Grace De Souza, kufariki, na anaendesha biashara hiyo na mumewe, Clarence Abranches ambaye ni mhasibu mstaafu.

Clarence Abranches akicheza. Picha/ Diana Mutheu

Kulingana na Maura, janga la corona limeathiri biashara yao sana pale ambapo walilazimika kuifunga kwa miezi sita na kuwasimamisha kazi baadhi ya wahudumu wao.

“Tumepoteza mapato katika miezi hizo sita ilhali bado tulikuwa tunahitajika kulipa kodi ya ardhi, maji na umeme,” akasema Maura wakati wa mahojiano na Taifa Leo katika baa hiyo.

Hata hivyo, Maura alifafanua kuwa kati ya wahudumu watatu waliokuwa wanafanya kazi pale, mmoja alihifadhi nafasi yake ya kazi.

“Hali ilitulazimu kuwasimamisha kazi wahudumu wawili, lakini tulichukua jukumu la kuwalipia kodi zao za nyumba na hata kuwanunulia vyakula kwa miezi hizo zote ambazo kazi yetu ilikuwa imesimama,” alisema Maura huku akiongeza kuwa wameanza mikakati ya kuhakikisha wanafungua tena hivi karibuni.

Wamiliki wa baa ya Kilindini, Maura De Souza Abranches (kulia) na Clarence Abranches. Picha/ Diana Mutheu

“Tukikamilisha kuweka mikakati yote ya kupigana na janga la corona, kama inavyotakikana na Wizara ya Afya, tutafungua baa hii tukiwa na matarajio kuwa tutapata wateja wengi wa humu nchini na hata kutoka nje. Tayari, baadhi ya wateja wetu wa mara kwa mara wameanza kutuma jumbe wakiuliza kama tumefungua, na hivyo tutaharakisha mipango yote inayotakiwa,” akasema Maura.

Kulingana na historia kama anavyoeleza Maura, baa hiyo ilijengwa mwaka wa 1908, wakati nchi ya Kenya haikuwa na kiwanda hata kimoja cha kutengeneza pombe, na nyingi ziliagizwa kutoka Afrika Kusini, Uropa na Japani, na chupa moja ya bia iliuzwa kwa senti 75.

Kwa miaka hiyo yote, baa hiyo imekuwa ikimilikiwa na familia moja tu inayojulikana kama De Souza.

Hali ya kawaida katika baa hiyo huwa na madhari yenye utulivu bila makelele na wateja wengi huwa ni wazee, lakini Maura alisema kuwa vijana pia hunywa pombe mle.

Vifaa vingi katika jengo hilo kuanzia viti, meza, picha zilizotundikwa ukutani, feni na simu zote ni za zamani.

Katika ukuta mmoja kumetundikwa picha za bia zilizouzwa mwaka wa 1928, na hata mabango mazee ya kutangaza vinywaji kama vile soda.

Pia, mabango ya sigara zilizovutwa miaka ya zamani, chupa za pombe zenye miundo ya kitambo bado zipo katika kaunta moja kubwa katika baa hiyo, zote zikiwekwa pale ili kuhifadhi historia kali.

Pia kuna saa moja iliyonunuliwa mwaka wa 1910 na lazima isetiwa upya kila wiki.

“Stuli na kaunta hiyo ni ya zamani sana na ilitengenezwa kwa mbao kutoka kwa mti wa mvule,” akasema mwanabiashara huyo.

Licha ya utulivu ulioko katika sehemu hiyo ya burudani, wateja wanaweza kucheza mchezo wa datsi na ‘pool’.

Kulingana na kijitabu chenye maelezo mafupi ya kimatangazo (brosha) ya baa hiyo, viongozi na watu wengine waliochangia ukuaji wa kisiwa cha Mombasa na bandari kwa jumla, walijumuika pale kujiburudisha na kuzungumzia ‘shida’ zao.

Baadhi ya viongozi waliotajwa kuzuru baa hiyo ni Ronald Ngala ambaye alikuwa kiongozi wa chama cha Kenya African Democratic Union (KADU), na mwandishi maarufu kutoka Amerika, Ernest Hemingway.

Mwanzilishi wa baa hiyo aliitwa Alex Caetano De Souza kutoka jamii ya Wagoa, India na alizuru Afrika Mashariki mwaka wa 1898, ambapo alifanya kazi ya ukarani katika kampuni moja ya kusafirisha bidhaa ya Smith Mackenzie & Company, na ofisi zao zilikuweko katika barabara ya Ndia Kuu, Old Town.

Maura alielezea kuwa zamani baa hiyo ilizingirwa na bustani nzuri na msitu mkubwa na wangeweza kuwaona baadhi ya wanyama. Lakini sivyo ilivyo hali ya sasa manake majengo ya kibiashara yamejengwa kote, hakuna msitu tena.

Alisema kuwa babu yake, Bw De Souza alitumia toroli kama mbinu kuu ya usafiri kutoka eneo moja hadi lingine.

Zaidi aliguzia kuwa katika enzi za ukoloni, wateja wengi katika baa hiyo walikuwa Wazungu na Wahindi, kwani Waafrika hawakuruhusiwa pale.

“Baba yangu alitusimulia kisa kimoja ambapo alitozwa faini ya Sh4,000 kwa kumpa bia mteja mmoja mwenye asili ya Kiafrika. Hizo zilikuwa pesa nyingi katika enzi hizo,” akasema Maura.

Pia, wateja wengi walikunywa pombe na kulipa deni zao mwisho wa mwezi.

“Hiyo haikuwa mbinu nzuri ya kufanya biashara kwa kuwa wateja wengi walitoroka bila kulipa madeni,” akasema.

Maura na mumewe, Clarence wana maono ya kuendelea kuhifadhi historia ya baa hiyo ili wateja wao waendelee kufurahia mandhari ya kikale.

Zaidi, baadhi ya vitu vinavyotumia teknolojia ya kisasa katika baa hiyo ni televisheni ambayo wateja huangalilia mchezo wa kandanda.

“Tunakazana tufungue ili wageni waweze kututembelea,” akasema Maura.