Michezo

Baada ya mabeki wawili kwa mpigo, Ten Hag sasa awinda kiungo Man U ikifungua msimu EPL Ijumaa

Na CECIL ODONGO August 16th, 2024 1 min read

KOCHA wa Manchester United Erik ten Hag amesema kuwa ana matumaini ya kumsajili kiungo mmoja kabla kipindi cha uhamisho wa wachezaji kukamilika.

Ten Hag hasa ameelekeza macho kwa Manuel Ugarte wa PSG na Sander Berge wa Burnley.

Hata hivyo, inadaiwa uongozi wa United umekuwa vuguvugu katika kuwasajili wawili hao kutokana na bei ya juu ambayo wamewekewa.

Tayari Napoli wanaandama kiungo wao McTominay ambaye United imesema ipo radhi kumuuza kwa kima cha Sh4.1 bilioni.

Wamiliki wa Man United tayari wametumia Sh23 bilioni kuwanunua Joshua Zirkzee, Lenny Yoro, Matthijs de Ligt na Noussair Mazroaui.

Katika juhudi za kumsaka kiungo mwengine, Ten Hag sasa ameelekeza macho kwa Youssouf Fofana, 25.

Hii ni kwa sababu kuna pengo katika safu ya kati ambapo Mbrazil Casemiro, 32 ameachwa pekee yake ndiposa kocha huyo anasaka kiungo mkali.

Vyombo habari nchini Italia vimeripoti kuwa Fofana ataigharimu United Sh4.3 bilioni japo pia anaandamwa na AC Milan, mabingwa wa zamani wa Italia.