Habari za Kitaifa

Baada ya minofu, hiki hapa Amerika inataka kutoka Kenya

May 25th, 2024 2 min read

Na CHARLES WASONGA

JAPO Kenya imevuna pakubwa kutokana na ziara ya Rais William Ruto nchini Amerika, taifa hilo pia linalenga kufaidi kwa kutumia Kenya kuendeleza masilahi yake ukanda wa Afrika Mashariki na pia upembe wa Afrika.

Wadadisi wa masuala ya diplomasia na mahusiano ya kimataifa wanasema ziara ya Ruto inailetea Amerika faida kubwa katika nyanja ya siasa, biashara, diplomasia, kijeshi, vita vya kupambana na ugaidi miongoni mwa manufaa mengine.

Aidha, wanasema Amerika inatumia ziara hiyo kuendeleza ushawishi wake nchini Kenya na bara la Afrika kwa ujumla “ikizingatiwa kuwa Rais Ruto amejitokeza kama mtetezi sugu wa masilahi ya Afrika.”

“Kwanza kabisa, kumbuka kwamba huu ni mwaka wa uchaguzi wa urais nchini Amerika. Hii ndio maana utawala wa Biden umemwalika Ruto na kuratibu kwamba atue kwanza mjini Georgia, jimbo la Atlanta, lenye idadi kubwa ya Waamerika weusi. Chama tawala cha Democrat kinapania kuonyesha kuwa kinajali Afrika na watu weusi,” anasema Masibo Lumala.

“Hii inatokana na hali kwamba, Rais Biden alifeli kuzuru Afrika alivyoahidi mnamo 2023 na hivyo kutoa taswira ya kiongozi asiyejali bara hili lenye umuhimu mkubwa katika sera za kigeni za Amerika,” anaongeza Profesa Lumala ambaye anafundisha kozi ya Diplomasia na Mahusiano ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Moi.

Rais William Ruto na mwenzake wa Amerika Joe Biden baada ya mkutano wa pamoja na waandishi habari katika White House, Washington, D.C. Picha|PCS

Amerika pia inalenga kufaidi kutoka kwa Kenya kuhusiana na mpango wa kuleta amani nchini Haiti na kurejeshwa kwa utawala wa kidemokrasia katika taifa hilo la Carribean.

Mwaka jana, Kenya iliidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) kuongoza shughuli za kuleta amani nchini Haiti kwa kutuma maafisa 1,000 wa polisi watakaosaidiana na polisi nchini humo kupambana na magenge ya wahalifu.

“Amerika ndio inatoa ufadhili wa kifedha na kimafunzo kwa mchakato huo ili kufanikisha masilahi yake ya kufyonza utajiri wa madini nchini Haiti,” Profesa Lumala anaeleza.

Kwa upande wake, Profesa Macharia Munene asema Amerika imealika Rais Ruto baada ya kutishiwa na hatua ya Rais Ruto kuweka mikataba ya ushirikiano wa kibiashara na mataifa mengine kama China na Urusi pamoja na miungano ya kiuchumi kama vile Jumuiya ya Ulaya (EU).

“Kwa mfano, mwaka jana, Kenya ilitia saini Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi (EPA) na EU. Aidha, mnamo Februari mwaka huu, Kenya ilikamilisha mazungumzo ya mkataba wa kibiashara kati yake na Umoja wa Milki za Kiarabu (UAE).

“Isitoshe, Amerika inapania kufaidi kwa kuiweka Kenya karibu ili utawala wa Rais Ruto usiamue kuegemea zaidi nchini China alivyofanya mtangulizi wake Uhuru Kenyatta,” anaeleza Profesa Munene ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Amerika-tawi la Kenya.

Kwa mtazamo wake, Amerika imejitolea kufadhili mradi wa upanuzi wa barabara kuu ya Nairobi-Mombasa ili ishindanie manufaa ambayo China imepata kupitia ujenzi wa miundo msingi nchini, haswa reli ya SGR.

“Miradi ya ujenzi wa barabara, reli na miundo msingi mingine nchini iliyofadhiliwa na China nyakati za utawala wa Uhuru ilifaidi pakubwa kampuni zake haswa katika nyanja za kiufundi, hali ambayo haikufurahisha Amerika,” anaeleza Profesa Munene.

Rais Biden pia aliamua kupandisha Kenya hadhi kuwa mshirika mkuu asiye mwanachama wa kundi la kujihami la NATO, hatua inayoonekana kulenga kuendeleza masilahi ya Amerika.

Sababu ni kwamba, hatua hiyo itaiwezesha Amerika kuiuzia Kenya silaha wakati huu ambapo serikali inaendesha mpango wa kuimarisha nguvu za vikosi vya usalama kupambana na magaidi na wahalifu wengineo.

Amerika pia ina kituo cha kijeshi katika eneo la Pwani kinachoisadia katika vita dhidi ya ugaidi ukanda huu.