Habari Mseto

Baada ya Uganda kukamata polisi 3 wa Kenya, Kenya nayo yakamata raia 53 wa Uganda

June 13th, 2018 1 min read

Na GAITANO PESSA

POLISI mjini Busia wanawazuilia watu 53 wanaoshukiwa kuwa raia wa Uganda kwa kuwa nchini kinyume cha sheria.

Kundi hilo ambalo lilijumulisha wanaumme, wanawake na watoto linazuiliwa katika kituo cha polisi cha Busia baada ya kunaswa katika eneo la Bumala, takriban kilomita 20 kutoka mpaka wa Kenya na Uganda.

Wengi wao hawakuwa na stakabadhi zinazowaruhusu kuingia nchini huku idadi kubwa ikiwa inafahamu lugha ya Kiganda inayozungumzwa zaidi katika taifa hilo.

Kamanda wa polisi katika gatuzi la Busia, Wambua Katiithi alisema washukiwa hao, ambao baadhi yao walikuwa na stakabadhi bandia, walinaswa katika eneo hilo kufuatia msako ulioendeshwa na polisi kwa ushirikiano na Idara ya Uhamiaji.

“Nia yetu ilikuwa kuwanasa wale wanaosafiri bila stakabadhi muhimu kama vile vitambulisho na pasipoti kutoka kwa idara ya uhamiaji. Tutaendeleza msako huku na wale waliokamatwa watafikishwa mahakamani kujibu mashataka ya kuwa nchini kinyume cha sheria.

“Uchunguzi wetu wa mapema umefichua kuwa wengi wa walionanswa ni wale waliodanganywa kuwa wanaingia nchini kutafutiwa ajira kama wajakazi. Hii ni dhuluma dhidi ya watoto na utapeli,” alisema bw Katiithi

Bw Katithi alifichua kuwa washukiwa hao walikuwa safarini kuelekea jijini Nairobi.